Na mwandishi wetu, Gazetini
KATIKA sehemu ya kwanza, tuliona mwandishi wa habari wa Marekani, Miller, akimuuliza Osama kilichomsukuma kuacha utajiri wake na kuingia kwenye uwanja wa vita dhidi ya Umoja wa Kisoviet.
Tukasema kabla ya kusikia jibu kutoka kwa Osama, ni vyema kupata historia kidogo juu ya Osama na Umoja wa Kisoviet. Tuanzie hapo. Endelea …
Osama alizaliwa Saudi Arabia akiwa mmoja ya watoto 20 wa tajiri wa sekta ya ujenzi, Muhammad bin Laden, ambaye kupitia kampuni yake ya Bin Laden Group alikuwa na utajiri wa Dola milioni 5.
Ukaribu wake na familia ya kifalme ya Saudi ulimuwezesha Muhammad bin Laden kupata mikataba mingi ya serikali ya ujenzi wa barabara katika maeneo ya mijini na hata majangwani.
Kutokana na ukwasi wa mzee wake, haikushangaza kuona Osama akisoma vizuri jijini London, Uingereza.
Hata hivyo, baada ya Umoja wa Kisoviet kuivamia Afghanistan mwishoni mwa mwaka 1979, Osama akiwa na umri wa miaka 22 tu aliondoka Saudia. Alikwenda Afighanistan kuisaidia kwenye vita dhidi ya ‘maadui’ zao hao.
Kama ilivyoelezwa hapo juu kwamba baba yake alikuwa tajiri mkubwa, Osama alitumia fedha zake kuajiri, kusafirisha na kuwanunulia silaha maelfu ya Wapalestina, Watunisia, Wasomali, Wamisri, Wasaudia na Wapakistan waliokuwa wakiisaidia Afighanistan.
Kwa Osama, kutoa fedha pekee haikutosha, bali pia alikuwa mstari wa mbele kwenye uwanja wa vita akiendesha magari yaliyobeba wapiganaji.
Je, kwanini aliacha kuishi kitajiri na kuingia vitani? Sasa tunaweza kusikia alichosema Osama kumjibu Miller katika swali hilo. “Ni ngumu kwa mtu ambaye si Muislam kuelewa.
“Wakati wa vita za jihad, maelfu ya vijana waliokuwa na fedha nyingi waliyaacha maeneo yao na kwenda vitani. Mamia waliuawa Afghanistan, Bosnia na Chechnya.
Akielezea ugumu wa vita dhidi ya Umoja wa Kisoviet, Osama alisema: “Tulipitia vita ngumu dhidi ya Warusi. Warusi wanafahamika kwa namna walivyo makatili.
“Walitumia hata gesi za sumu dhidi yetu. Tulipoteza wapiganaji wengi. Lakini tuliweza kutekeleza mashambulizi mengi ya kikomando kuliko wakati mwingine wowote.”
Katika swali lake la pili kwa Osama, Miller alitaka kujua chanzo cha uadui wake na Marekani, pia akimuuliza kama anahofia kwamba ipo siku atakamatwa.
“Mmarekani anapenda kuwa juu ya kila mtu. Wamarekani wanawashutumu watoto wetu wa Palestina kwa ugaidi. Watoto ambao hawana silaha wala hawana ukomavu wa akili.
“Vikwazo vinavyoongozwa na Marekani vimesababisha vifo vya watoto zaidi ya milioni moja huko Iraq. Yote hayo yanafanyika kwa masilahi ya Marekani. Tunaamini kwamba wao ndiyo wezi na magaidi wakubwa zaidi hapa duniani.”
“Wakati huo huo, Wamarekani wanaikingia kifua nchi ya Wayahudi (Israel). Tuna uhakika kwamba Mtume ametuhakikishia ushindi wetu dhidi ya Marekani na Israel. Siku ya mwisho haitofika hadi pale Uislam utakapouangusha uyahudi …”
Usikose sehemu ya tatu ya makala haya … Tembelea www.gazetini.co.tz.


