Na mwandishi wetu, Gazetini
MWANDISHI wa habari wa kituo cha televisheni cha ABC cha Marekani, John Miller, anasimulia mahojiano aliyofanya Mei, 1998, na aliyekuwa kiongozi wa Al-Qaeda wakati huo, Osama Bin Laden.
Mahojiano yaliyofanyika kwa dakika 60 baada ya Miller kumuibukia Osama ambaye wakati huo alikuwa mafichoni huko Kusini mwa Afghanistan.
Ni mahojiano yaliyofanyika kiasi cha miezi miwili tu kabla ya Al Qaeda kushambulia ofisi za balozi mbili za Marekani zilizoko Nairobi (Kenya) na Dar es Salaam (Tanzania) katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika simulizi yake iliyochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1999, Miller anaanza kwa kueleza mazingira magumu aliokutana nayo katika maficho ya Osama, ikiwamo mpigapicha wake, Rick Bennett, kupokonywa kamera.
“Walimpa kamera yao aina ya Panasonic,” anasema Miller akiongeza kuwa ulinzi ulikuwa mkali katika kambi hiyo, huku kila mlinzi akiwa na bunduki yake aina ya AK-47.
Baada ya kupewa kamera hiyo, Miller na Bennett walisogea aliko Osama, tayari kwa ajili ya mahojiano. Miller anasema: “Alikuwa amezungukwa kamanda wa jeshi, Muhammad Atef na nyuma yake alikuwepo Ayman al-Zawahiri, kiongozi wa Kundi la Kiislam la Misri lililokuwa limeungana na Al Qaeda.”
Kwa mujibu wa Miller, Bin Laden aliyekuwa mrefu kuliko wenzake hao, alimsogelea na kumwelekeza kibanda kilichokuwa karibu, ambacho ndicho kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya mahojiano.
Kama ishara ya heshima kwa Osama, mmoja ya walinzi waliokuwa kwenye kibanda hicho alianza kumimina risasi nyingi hewani, kisha wengine wakafuata, kwa mujibu wa Miller akiendelea kusimulia.
“Ndipo tukaingia kibandani. Mbali na urefu wake, kingine kilichonishangaza kuhusu bin Laden ni sauti yake. Alikuwa na sauti nyororo, ya chini na yenye utulivu, ambayo ungeweza kuifananisha na anayotumia mjomba kutoa ushauri kwa kijana wake,” anasema Miller.
Miller anaongeza kuwa ndani ya chumba kilichopigwa rangi nyeupe, Bin Laden akiwa amevaa jaketi lake maarufu la kijeshi, alikaa chini, kisha bunduki yake ya AK-47 ikiwa nyuma yake, yaani ikiegemea ukutani.
“Wasaidizi wake 20 nao walikuwepo pale chumbani, wakiwa makini kusikiliza kila kilichokuwa kikizungumzwa. Tayari tulishatanguliza maswali siku moja kabla kama walivyotaka wasaidizi wake,” anasema Miller.
Dakika chache tu baada ya salamu, msaidizi wa Osama alisema kumwambia Miller na Bennetti kwamba kiongozi wao huyo amekubali kujibu maswali yote, pasi na kuacha hata moja.
Kwa kuwa Miller hakujua Kiarabu, lugha aliyokuwa akitumia Osama, alikuwepo mtu maalumu kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano ya pande mbili hizo kwa kutafsiri.
Katika swali lake la kwanza kwa Osama, Miller alitaka kufahamu kwanini aliamua kuachana na maisha ya kitajiri ya familia yake na kuchagua tabu za vita dhidi ya Umoja wa Kisoviet?
Kabla ya kusikia jibu, ni vizuri kupata historia kidogo juu ya Osama na Umoja wa Kisoviet. Tukutane katika sehemu inayofuata … Tembelea www.gazetini.co.tz.


