22.5 C
New York

Mkataba wa mafuta na Marekani; faida au hasara kwa Venezuela?

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

MAREKANI imeuita kuwa ni ‘mkataba bora zaidi wa mafuta katika historia ya dunia’. Ni mkataba unaoipa Marekani sehemu ya akiba ya mafuta ya Venezuela. Makubaliano hayo yanafikiwa ikiwa ni miezi nane imepita tangu Marekani ilipovamia nchini humo na kumng’oa Ikulu aliyekuwa Rais wake, Nicolas Maduro.

Kwa upande wake, Rais wa Mpito wa Venezuela, Delcy Rodriguez, amesema mkataba huo wa kuipa Marekani sehemu ya akiba ya mafuta unakwenda kuinua uchumi wa nchi yake, pamoja na kuboresha sekta ya nishati ya mafuta.

Je, mkataba huo ukoje? Marekani kwa kushirikiana na shirika binafsi la Venezuela (jina halijatajwa) zimeunda kampuni, ambayo imepewa haki ya kushughulika na akiba ya mafuta ya nchi hiyo ya Amerika ya Kusini kwa miaka 100.

Huku Marekani ikitarajiwa kuvuna mapipa bilioni 65, sekta ya mafuta ya Venezuela itafaidika na uwekezaji mpya wa Dola bilioni 100, wakati huo ikiingiza mapato ya kodi yanayotarajiwa kufikia Dola bilioni 209.

RAIS APINGANA NA RAIA VENEZUELA

Akizungumzia mkataba huo, Rais Rodriguez amesema: “Jambo linalopaswa kueleweka hapa ni kwamba Venezuela itaendelea kuwa mmiliki na yenye mamlaka kamili ya rasilimali zake.”

Hata hivyo, kwa baadhi ya raia wa Venezuela, wanauona mkataba huo kuwa ni usaliti wa wazi wa Rais wa Mpito, Rodriguez, dhidi ya nchi yao. Wengi wao wanaona Serikali ya sasa inaimilikisha Marekani rasilimali za Taifa lao.

Douglas Borjas, mkazi wa Mji Mkuu wa Caracas, ni miongoni mwa wananchi walioleza kusikitishwa na hicho kilichoitwa ‘mkataba bora zaidi wa mafuta kuwahi kutokea katika historia ya dunia’.

Kwa mujibu wake, Rais Rodriguez ‘anauza’ rasilimali kwa Marekani ili ilimlinde kubaki madarakani, labda akihofia kile kilichomkuta mtangulizi wake, Maduro, ambaye si tu alitolewa madarakani kwa mtutu wa bunduki, bali pia alipelekwa Marekani na kufunguliwa mashitaka.

“Watu wa Venezuela wanastahili kuishi vizuri. Venezuela ina rasilimali zinazopaswa kutumika, lakini kwa masilahi ya watu wake, siyo kwa masilahi ya tabaka la rushwa,” amesema Borjas.

Wakati huo huo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Harvard, Ricardo Hausmann, ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mipango wa Venezuela, ameuita mkataba huo kuwa ni aibu.

“Watu wa Venezuela hawatoheshimu mkataba huu haramu na hakuna kampuni kubwa ya mafuta ya Marekani itakayouchukulia kwa uzito kwa sababu zinajua kabisa kwamba si wa muda mrefu,” amesema Prof. Hausmann.

MAREKANI NAO WATOFAUTIANA

Washirika wa Rais Donald Trump nchini Marekani wameuita mkataba huo na Venezuela kuwa ni ‘ushindi mkubwa’. Seneta wa Ohio, Bernie Moreno, amesema ni mkataba wa kihistoria na wenye tija kwa pande zote mbili (Marekani na Venezuela).

“Kama ingekuwa Democrat (wapinzani wa Republican ya Trump), Maduro angekuwa madarakani hadi leo hii. Mafuta ya Venezuela yangekuwa yanakwenda China kwa nusu bei, na watu wa Venezuela wangekuwa wanaendelea kunyonywa na utawala uliojaa rushwa,” amesema Moreno.

Hata hivyo, mkataba huo unapondwa vikali na wanasiasa wa upinzani, Democrat, ambao wanasema ‘uchu’ wa Rais Trump uko kwenye utajiri wa mafuta walionao Venezuela. Kwamba hata kumtoa Maduro madarakani kulitokana na hilo.

Kwa walio wengi, akiwamo Seneta Chris Van Hollen, Trump anayatolea macho mafuta ya Venezuela ili kuwatajirisha mabilionea wake walioko ndani na nje ya mfumo wa serikali anayoiongoza.

Related articles

Recent articles