TOKYO, Japan
MVUA kubwa iliyonyesha usiku wa jana Agosti 13, 2026, huko Chiba, jirani na Mji Mkuu wa Tokyo, imesababisha vifo vya watu wanne, huku ikiathiri upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo mengi.
Takwimu rasmi zinaonesha kuwa Chiba imepokea kiwango cha mvua cha zaidi ya milimita 100 kuanzia jana. Ni mara tatu ya mvua zinazonyesha Agosti ya kila mwaka.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni mwanamke aliyekuwa kwenye gari lililosombwa na maji, kwa mujibu wa taarifa za mamlaka.
Kwa mujibu wa mamlaka za Tokyo, wakazi zaidi ya 20,000 wamekosa umeme, pia mvua ikisababisha adha kubwa kwa wasafiri 7,000 katika Uwanja wa Ndege wa Narita.
Aidha, katika utabiri wake, Mamlaka za Hali ya Japan imetahadharisha kuwa mvua hizo zitaendelea kunyesha kwa siku kadhaa zijazo.
Kwa upande wake, Gavana wa Chiba, Toshihito Kumagai, amedai kuwa mvua hiyo imevuka kiwango kilichotarajiwa na ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Japan.
“Nimeshuhudia majanga mengi hapo nyuma, lakini sijawahi kuona kilichotokea safari hii,” amesema Gavana huyo.


