30 C
New York

Sekta za Mageuzi zinazoibeba Dira 2050: Kilimo

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

DIRA 2050 inaanisha vigezo vitano vya kuchagua sekta za mageuzi. Vigezo hivyo vinatokana na umuhimu na mchango ambao umekuwa ukitolewa na sekta hizo katika uchumi wa nchi.

Sekta ambazo zimekuwa zikizalisha ajira kwa wingi, kuongeza mauzo ya nje, kukua yenyewe na kuchochea ukuaji wa sekta zingine, kuongeza thamani, na kukuza mapato ya Serikali.

Moja ya sekta hizo ni kilimo inayojumuhisha mazao, mifugo, uvuvi na misitu, ambayo imekuwa ikichangia asilimia 26.5 ya Pato la Taifa, ikiajiri asilimia 65 ya nguvukazi na kuzalisha asilimia 30 ya mapato ya nje.

Wakati huo huo, uhusiano wake mkubwa na sekta za viwanda, usafirishaji na biashara unabainisha nafasi yake katika kukuza ajira na uchumi.

Kufikia mwaka 2050, sekta hiyo inatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa, yenye tija, endelevu na yenye ushindani wa hali ya juu. Hii itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha chakula katika Ukanda wa Afrika.

Hivyo basi, mageuzi yanahitajika katika kila sekta ndogo ya kilimo: sekta ya mazao itaweka mkazo kwenye mazao yenye thamani kubwa sokoni.

Pili, sekta ya mifugo nayo itaboreshwa kwa kuwekeza katika uzalishaji wa kisasa wa bidhaa zinazotokana na mifugo kwa kuongeza tija na thamani ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.

Tatu, sekta ya uvuvi itaimarishwa kwa kuendeleza uvuvi na ufugaji wa Samaki; usimamizi wa mazao ya uvuvi na miundombinu baridi ya uhifadhi na usafirishaji.

Nne, sekta ya misitu inahitaji inahitaji mikakati thabiti ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu, pamoja na kuendeleza biashara ya mazao ya misitu na upandaji wa miti kibiashara.

Hata hivyo, mafanikio ya mageuzi ya sekta ya kilimo yanahitaji uwekezaji mkubwa katika teknolojia ya kisasa, miundombinu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na programu za kuwawezesha wakulima kukuza biashara zao.

Vilevile, ni muhimu kuwekeza katika nishati nafuu, upatikanaji wa fedha, upanuzi wa mitandao ya masoko na kuhimiza mbinu endelevu za kilimo.

Kwa pamoja, mikakati hii itasaidia kujenga sekta ya kilimo iliyo imara, jumuishi, na yenye ushindani wa kimataifa. Sekta itakayoweka msingi wa ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Related articles

Recent articles