26 C
New York

Peter Shalulile amekuja na viatu vyake vya mabao?

Published:

Na Hassan Mwasha

KATIKATI ya ushindani wa Kaizer Chiefs, Orlando Pirates, Scottland FC na Pyramids, Yanga imeweza kumnyakua straika aliyeondoka Mamelodi Sundowns, Peter Shalulile.

Yanga wameishitua Tanzania kwa usajili wa straika huyo, ikielezwa kuwa wametumia Dola za Marekani 700,000 (zaidi ya Sh bil. 1.8 za Tanzania) kumshawishi asaini mkataba wa miaka miwili.

Shalulile raia wa Namibia, ametua Yanga kwa ushawishi wa kocha aliyekuwa naye Mamelodi, Manqoba Mngqithi, ambaye naye yuko Jangwani.

Aidha, baada ya miaka sita ya kucheza Mamelodi, ameondoka akiwa mchezaji huru kuja kuziba pengo la Prince Dube, hivyo kuungana na Laurindo Aurelio ‘Depu’ na Hussein Mihambo katika safu ya ushambuliaji ya Yanga.

Swali la msingi; je, Shalulile mwenye umri wa miaka 32 amekuja Bongo na viatu vyake vya mabao au ameviacha Afrika Kusini?

Iko hivi; nyota huyo ameondoka Mamelodi akiwa ameacha historia ya kuvutia ya upachikaji mabao. Katika hilo, waulize mashabiki wa klabu hiyo.

Hadi anaondoka Mamelodi kwa ridhaa yake baada ya majeraha kumtesa msimu uliopita (2025-26), Shalulile alishaingia kambani mara 107 katika mechi 228 tu za mashindano mbalimbali.

Wakati huo huo, mkali huyo ameiacha Ligi Kuu ya Afrika Kusini akiwa ndiye mfungaji bora wa muda wote baada ya kuzifumania nyavu mara 132.

Kwamba ni mchezaji wa nne wa Mamelodi kufunga mabao 100 au zaidi katika Ligi, akiungana na wakongwe Siyabonga Nomvethe, Collins Mbesuma na Daniel Mudau, ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo.

Pia, Shalulie ana historia ya kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika, akifanya hivyo mwaka 2023, pia akibeba mara tatu kwa upande wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Vilevile, ukali wake wa kuzipasia nyavu umempatia tuzo nyingi akiwa Sauzi, ikiwamo ya Mchezaji Bora wa Mwaka Ligi Kuu (2020-21 na 2021-22).

Lakini je, ataendeleza makali yake hayo akiwa na Yanga? Ni swali gumu, ikizingatiwa kuwa wakati mwingine mazingira mapya yanaweza kuwa changamoto kwa mchezaji kuendeleza ubora wake.

Related articles

Recent articles