NEW YORK, Marekani
MIAKA 10 iliyopita, Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la kumaliza aina zote za umasikini, kuhakikisha usawa katika jamii, pamoja na kudhibiti majanga yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kupitia Mpango wake wa Maendeleo Endelevu, UN ilijiwekea malengo 17 ya kufikiwa ifikapo mwaka 2030, ikiwamo kumaliza janga la njaa, upatikanaji wa maji safi, huduma bora za afya, na matumizi ya nishati safi.
IKIWA ni miaka mitatu imebaki, hali ikoje? Kwa ufupi, bado umasikini umeonekana kuwa changamoto kubwa duniani.
Kwa takwimu, kati ya watu 10 duniani, mmoja anaishi kwenye shimo la umasikini uliotopea, huku zaidi ya bilioni mbili, sawa na asilimia 8, wakiwa na hali isiyoridhisha ya usalama wa chakula.
Wakati huo huo, idadi ya walioathiriwa na majanga yatokanayo na hali ya hewa, mathalan ukame, imeongezeka mara mbili tangu wakati wa kuasisiwa kwa Mpango huo wa Maendeleo Endelevu mwaka mwaka 2015.
UN inakiri kuwa kati ya watu wanne walioko maeneo ya mijini, mmoja anaishi kwenye vibanda au makazi yasiyo rasmi.
Wakati huo huo, licha ya upatikanaji wa maji safi kuongezeka, ikilinganishwa na mwaka 2024, bado huduma hiyo haiko karibu na watu katika maeneo mengi.
Kwa mujibu wa takwimu, asilimia 10 ya watu duniani wanapata msongo wa mawazo juu ya umbali au upatikanaji wa mara kwa mara wa huduma ya maji.
Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yamechangia kukauka kwa mito mingi, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo la maji.
Wakati huo huo, dunia inaendelea kushuhudia watu wake zaidi ya milioni 650 wakiwa hawajafikiwa na huduma ya nishati ya umeme, asilimia 86 wakiwa ni raia wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.
Aidha, wakati dunia ikijivunia kupungua kwa majanga ya asili, mathalan matetemeko ya ardhi, idadi ya waathirika imeongezeka, kwa mujibu wa takwimu za UN.


