MIAMI, Marekani
HISTORIA inarudisha kilichotokea miaka 16 iliyopita, ambapo timu ya soka ya taifa ya Hispania ilitwaa ubingwa wa Kombe la Dunia ikiwa kwenye ardhi ya Afrika Kusini.
Msimu huu, chini ya kocha De la Fuente, mabingwa hao wa EURO 2024 walianza safari yao kwa suluhu (0-0) dhidi ya timu mpya kwenye historia ya Kombe la Dunia, Cape Verde.
La Roja walikutana na Saudi Arabia katika mchezo uliofuata na kupata ushindi wa mabao 4-0, kabla ya kuvuka makundi kwa kuifunga Uruguay bao 1-0.
Katika hatua ya 32 Bora, Hispania walikuta na Austria kupata ushindi mnono wa mabao 3-0, siku ambayo Mikel Oyarzabal alizipasia nyavu mara mbili.
Hatua ya 16 Bora iliwakutanisha Ureno ya Cristiano Ronaldo. Licha ya ugumu wa mechi, Hispania ilichomoza na ushindi wa bao 1-0.
Baada ya matokeo hayo, walikutana na Ubelgiji katika hatua ya robo fainali na kuondoka na ushindi wa mabao 2-1.
Nusu fainali nayo ilikuwa ngumu kwani walikutana na Ufaransa. Hispania wakashinda mabao 2-0 dhidi ya mabingwa hao wa Kombe la Dunia mwaka 1998 na 2018.


