MIAMI, Marekani
ANAITWA Slavko Vincic, mwamuzi wa kati aliyeteuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kucheza mechi ya fainali msimu huu wa Kombe la Dunia (2026).
Mchezo wa Julai 19, 2026, utakaozikutanisha Argentina na Hispania katika Uwanja wa MetLife nchini Marekani.
Vincic (46), anakuwa mwamuzi wa kati wa kwanza raia wa Slovenia kuchezesha fainali ya Kombe la Dunia. Pia, ni refa wa 23 kupewa fainali tangu michuano hiyo ilipoanzia mwaka 1930.
KAULI YAKE
Baada ya kutaarifiwa na Mwenye kiti wa Kamati ya Waamuzi ya FIFA, Pierluigi Collina, kwamba atachezesha fainali, Vincic alisema:
“Kwanza, imenishitua. Pili, nimefurahi. Ni heshima kubwa kupewa fainali ya Kombe la Dunia. Ni ndoto pekee aliyonayo kila mwamuzi anapoanza kazi hii …”
“Ni ngumu kusema kila kitu lakini ninefurahi kuiwakilisha nchi yangu, Slovenia, katika tukio hili kubwa zaidi katika michezo.”
Huu ni msimu wa pili kwa refa huyo kuchezesha michuano ya Kombe la Dunia baada ya kusimamia mechi mbili mwaka 2022 nchini Qatar.
Msimu huu, alipuliza kipyenga katika mechi tatu; Brazil na Morocco, Algeria dhidi ya Jordan, na Mexico ilipokutana na Ecuador.
Amekuwa refa anayetambulika na FIFA tangu mwaka 2010 na Argentina dhidi ya Hispania siyo mechi kubwa pekee aliyowahi kuchezesha katika maisha yake ya uamuzi.
Kama itakumbukwa, Vincic ndiye aliyechezesha fainali ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League) kati ya Frankfurt na Rangers mwaka 2022.
Mwaka 2024, Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) lilimpa fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund. Mechi ilichezwa Wembley na Madrid kushinda mabao 2-0.
Kwa mchezo huo, akawa refa wa pili kutoka Slovenia baada ya Damir Skomina (2019) kuchezesha fainali ya mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Ulaya.
Februari 24, 2025, Vincic alikuwa nchini Uturuki kuchezesha mchezo kati ya vigogo Fenerbahce na Galatasaray.
Miezi miwili baadaye, aliibukia Marekani kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu. Alichezesha River Plates dhidi ya Monterrey, ambapo alimwaga kadi za njano tisa na nyekundu moja.


