29.3 C
New York

DIB ilivyojenga imani ya wananchi kwenye benki hata zinapofilisika

Published:

Na Esther Mnyika, Gazetini

KWA Watanzania wengi, kuweka fedha benki ni njia salama ya kutunza akiba, kufanya miamala na kupanga mustakabali wa kifedha. Hata hivyo, swali ambalo huibuka mara kwa mara ni; nini hutokea iwapo benki itafungwa au kufilisika? Je, fedha za mteja hupotea?

Jibu la swali hilo linapatikana kupitia Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board – DIB), taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mahsusi kulinda fedha za wenye amana na kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa benki nchini.

Kupitia Mfumo wa Bima ya Amana, fedha za wateja walioweka akiba katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hulindwa pale taasisi hizo zinaposhindwa kuendelea na shughuli zake kutokana na kufungwa au kufilisika.

Mfumo unaolinda fedha za wananchi

Bodi ya Bima ya Amana ilianzishwa chini ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991 na kuanza shughuli zake rasmi mwaka 1994. Kwa sasa inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha Na. 5 ya mwaka 2006, kifungu cha 36 hadi 42.

Majukumu yake makuu ni kusimamia Mfuko wa Bima ya Amana, kulipa fidia kwa wenye amana, kusimamia ufilisi wa benki zinazofungwa na, tangu Julai 2025, kusaidia kupunguza hasara katika benki zinazokabiliwa na changamoto za kiuendeshaji ili ziweze kurejea kutoa huduma.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Mwandamizi wa DIB, Joyce Shala, alisema wananchi hawapaswi kuwa na hofu wanapoweka fedha zao benki kwa kuwa mfumo huo unawalinda kwa mujibu wa sheria.

Alisema zaidi ya asilimia 99 ya wenye akaunti nchini wanalindwa kwa asilimia 100 ndani ya kiwango cha fidia kinachotolewa na DIB.

“DIB hukusanya michango kutoka benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania, huwekeza fedha hizo kwenye dhamana za Serikali na kuzitumia kulipa fidia kwa wenye amana pale benki inapofungwa au kufilisika,” alisema Shala.

Huhitaji kujisajili

Shala alifafanua kuwa mwananchi hahitaji kufanya usajili maalumu ili kunufaika na Bima ya Amana.

Badala yake, mara tu anapofungua akaunti katika benki au taasisi ya fedha yenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania, moja kwa moja anakuwa chini ya ulinzi wa Mfumo wa Bima ya Amana.

Hali hiyo inaondoa wasiwasi kwa mamilioni ya Watanzania wanaotumia huduma rasmi za kifedha.

Benki huchangia mfuko wa bima

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, wanachama wa Mfuko wa Bima ya Amana ni benki na taasisi zote za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania zinazopokea amana za wananchi.

Alisema kila mwaka taasisi hizo huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana walizonazo.

Fedha hizo huwekezwa ili kuimarisha mfuko na kuhakikisha DIB inakuwa na uwezo wa kulipa fidia kwa wenye amana pamoja na kutekeleza majukumu mengine ya kisheria.

Kiwango cha fidia ni Sh milioni 7.5

Mwambande alisema kiwango cha juu cha fidia kinachotolewa kwa sasa ni Sh milioni 7.5 kwa mwenye amana katika benki moja.

Alisema kiwango hicho kilifikiwa baada ya tathmini kuonyesha kuwa idadi kubwa ya wenye akaunti nchini wana amana zisizozidi kiwango hicho.

Hivyo, mwenye amana ya kati ya shilingi moja hadi Sh milioni 7.5 hulipwa fedha zake zote kupitia Bima ya Amana pale benki inapofungwa.

Kwa wenye amana zinazozidi kiwango hicho, sehemu inayobaki hulipwa kupitia mchakato wa ufilisi wa benki husika kadiri mali zinavyorejeshwa.

DIB ndiyo msimamizi wa ufilisi

Mbali na kulipa fidia, DIB pia huendesha ufilisi wa benki zinazofungwa baada ya kuteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Lengo ni kukusanya na kuuza mali za benki kwa mujibu wa sheria ili wadai na wenye amana waliobaki waweze kulipwa stahiki zao.

Kwa sasa, DIB inaendesha ufilisi wa benki tisa.

Kati ya hizo, mbili zilifutiwa leseni mwaka 2000 na 2003, huku saba zikifutiwa leseni kati ya mwaka 2017 na 2018.

Mwambande alisema hatua za ufilisi katika benki hizo ziko katika viwango tofauti vya utekelezaji.

Mafanikio ya ufilisi

Kwa mujibu wa DIB, zoezi la ufilisi limeendelea kuzaa matokeo chanya.

Kwa mfano, hadi sasa wenye amana katika iliyokuwa FBME Bank wameshalipwa asilimia 85 ya fedha zinazotokana na mazao ya ufilisi.

Kwa upande wa Njombe Community Bank, wenye amana wamelipwa fedha zao zote.

Benki nyingine zinaendelea na hatua mbalimbali za ufilisi kwa mujibu wa taratibu za sheria.

Changamoto ya taarifa za wateja

Pamoja na mafanikio hayo, DIB inakabiliwa na changamoto ya kushindwa kuwafikia baadhi ya wenye amana kutokana na taarifa zao kupitwa na wakati.

Baadhi ya wateja hubadilisha namba za simu, anuani au taarifa nyingine bila kuzijulisha benki, hali inayochelewesha malipo ya fidia au mazao ya ufilisi.

Kutokana na hali hiyo, DIB imewataka wananchi kuhakikisha wanahuisha taarifa zao kila wanapofanya mabadiliko ili iwe rahisi kuwapata endapo kutahitajika.

Aidha, wananchi waliokuwa na akaunti katika benki zilizofungwa wanaweza kupata huduma za malipo kupitia matawi ya TCB Bank yaliyopo nchi nzima.

Elimu kwa umma yaendelea

Mbali na majukumu yake ya fidia na ufilisi, DIB inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia Maonesho ya Sabasaba, Nanenane, Wiki ya Huduma za Fedha, Maonesho ya Mapinduzi Zanzibar, Maadhimisho ya Muungano pamoja na kampeni mbalimbali za uelimishaji.

Lengo ni kuwahamasisha wananchi kutumia huduma rasmi za kifedha kwa kujiamini, wakifahamu kuwa fedha zao zinalindwa na Mfumo wa Bima ya Amana.

Kwa ujumla, DIB imeendelea kuwa moja ya taasisi muhimu katika kulinda maslahi ya wenye amana, kujenga imani ya wananchi katika sekta ya benki, kuimarisha uthabiti wa mfumo wa fedha na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia sekta salama na yenye kuaminika.

Related articles

Recent articles