Na mwandishi wetu, Gazetni
VIJANA wa Tanzania wametajwa kuwa kundi litakalobeba mafanikio makubwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku wakihimizwa kuanza kujijengea uwezo na kutumia fursa zinazotengenezwa kupitia mipango ya maendeleo ya Serikali.
Mchumi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Alpha Temu, ameiambia Gazetini kuwa katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, vijana wengi wamekuwa wakifika kwenye banda la Tume kuuliza nafasi yao katika utekelezaji wa Dira hiyo.
“Kinachonifurahisha ni kuona vijana wa miaka 15 hadi 20 wanakuja na kuuliza, ‘Sisi nafasi yetu ni ipi?’ Hilo linaonyesha wanaanza kuona kwamba wao ndio watakaokuwa watu wazima mwaka 2050,” amesema.
Ameeleza kuwa Serikali tayari imeweka msingi wa utekelezaji kupitia Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioanza Julai Mosi, ambao unalenga kuzalisha ajira, kuongeza ushindani wa uchumi na kuwezesha wananchi kujitegemea kiuchumi.
Tem amesema katika kipindi cha miaka 25 ijayo Tanzania inalenga kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja kwa kiwango kikubwa, jambo litakalohitaji mabadiliko ya fikra, kuongeza ujuzi na kutumia teknolojia katika uzalishaji.
“Teknolojia imebadilisha dunia. Kitu kilichokuwa kinachukua siku mbili sasa kinaweza kufanyika ndani ya saa chache. Hivyo tunahitaji kasi mpya ya kufikiri na kufanya kazi,” amesema.
Ameongeza kuwa mafanikio ya Dira hayatategemea sera pekee bali namna Watanzania watakavyobadili mtazamo wao kuhusu uzalishaji, ubunifu na matumizi ya fursa za kiuchumi.


