RIO, Brazil
UNAMKUMBUKA Alexandre Pato, kiungo wa zamani wa timu ya soka ya Taifa ya Brazil ‘Selecao’?
Alianza safari yake ya soka la kulipwa akiwa Internacional ya Brazil mwaka 2000, kabla ya kutua Ulaya akiwa na miaka 18 aliposajiliwa na AC Milan.
Moja ya alama kubwa alizoziacha akiwa Milan ni kufunga mabao 18 katika mechi 42 mwaka 2009 na kutwaa tuzo mbili za Kinda Bora (Ulaya na Serie A). Msimu uliofuata, 2010-11, akaipa ubingwa wa Serie A.
Klabu zingine alizowahi kucheza akiwa kwenye ubora wake ni Corinthians, Sao Paulo, Chelsea, Villarreal na Tianjin Quanjian ya China na Orlando City ya Marekani.
Nje ya uwanja, Pato ana stori ndefu ya warembo aliowahi kutoka nao, wote wakiwa ni maarufu ndani na nje ya Brazil.
Mwaka 2007, alikuwa na mwigizaji mwenye jina kubwa katika soko la filamu nchini Brazil, Sthefany Brito.
Waliachana miaka miwili baadaye, kabla ya kurudiana na kufunga ndoa ya kifahari katika fukwe za Copacabana mjini Rio de Janeiro.
Hata hivyo, ndoa yao ilidumu kwa miezi isiyozidi 10, wakaachana Aprili 21, 2010, huku bibiye Brito akisema chanzo ni Pato kupenda maisha ya kujirusha kwenye klabu za starehe.
Alipoachana na Brito, Pato alijiweka kwa mshindi wa Shindano la Urembo nchini Brazil kwa mwaka 2010, Debora Lyra. Hawakudumu.
Pato akaanza kuonekana na Barbara, ambaye ni binti wa aliyekuwa mmiliki wa AC Milan wakati huo, Silvio Berlusconi. Naye walidumu kwa miaka miwili na nusu tu.
Mwishoni mwa mwaka 2014, aliibukia kwa mwigizaji maarufu wa Brazil, Fiorella Mattheis, ambaye pia ni mtangazaji na staa wa tasnia ya mitindo nchini humo. Waliachana miaka mitatu baadaye.
Baada ya kuhangaika kote huko, Pato akanasa kwa Rebeca Abravanel, ambaye ndiye mke wake kwa sasa.
Rebeca, kwa wasiomfahamu, ni mtangazaji wa kituo cha televisheni cha SBT kinachomilikiwa na baba yake, Silvio Santos.
Katika kituo hicho, Pato naye ni miongoni mwa waajiriwa, ambapo amekuwa mchambuzi wa mechi za soka, kazi ambayo amekuwa akiifanya tangu Novemba, 2024.
Pia, tofauti na maisha ya awali ya kupenda kutoka usiku kwenda ‘kula bata’, staa huyo amebadilika. Anasema maisha yake yamekuwa na sura mpya tangu alipoanza kwenda kanisani.


