SERIKALI imekamilisha ujenzi wa madarasa 15,000 kwa asilimia 95 katika mikoa yote ya Tanzania bara, huku asilimia chache ikisalia kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo upatikanaji wa malighafi ya ujenzi na hali ya hewa.
Kupitia taarifa iliyotolewa hivi karibuni ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO -19 iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hadi kufikia Januari 15 madarasa hayo ujenzi wake utakuwa umekamilika kwa asilimia 100.
Kiasi cha sh bilioni 240 ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 12, 000 ya shule za sekondari na sh bilioni 60 kwa madarasa ya shule shikizi za msingi na sh bilioni 4 kwa ajili ujenzi wa mabweni 50 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Hadi kufikia Desemba 31, 2021 sekta ya elimu msingi Ofisi ya Rais TAMISEMI ilipokea sh bilioni 304 ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za Sekondari na shule shikizi jumla 15,000 pamoja na mabweni.
Ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari yatawezesha wanafunzi 907,803 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza, kuanza shule siku moja badala ya kuwa na awamu tatu kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
Ofisi ya Rais TAMISEMI iliomba madarasa 12,000 ikiwa na makadirio ya ufaulu wa asilimia 90 lakini matokeo ya ufaulu ni asilimi 82.
Kwa mujibu wa takwimu hizo kuna madarasa ya ziada 2,292 ambayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi wa vidato vingine kwa shule za Sekondari.
Ni wazi kuwa ujenzi wa madarasa hayo utaondoa changamoto ya wanafunzi wanaochelewa kuanza masomo ya kidado cha kwabnza kutokana na ufinyu wa madarasa, kwani takwimu zinaonyesha kuwa kwa takribani miaka sita kumekuwa na mfululizo wa wanafunzi wanaokosa vyumba vya madarasa kama inavyo katika jedwali letu hapa chini.
Mwenendo wa wanafunzi waliokuwa wakikosa nafai kidato cha kwanza sababu ya uhaba wa madarasa
Mwaka | 2016 | 2017 | 2018 | 2019 | 2020 | 2021 |
Wanafunzi | 12,847 | 28,638 | 11,173 | 133,747 | 59,765 | 74,166 |
Zaidi angalia uchambuzi kupitia usanifu wetu hapo juu.