31.1 C
New York

Unaifahamu Siku ya Mitandao ya Kijamii duniani?

Published:

LOS ANGELES, Marekani

JUNI 30 ya kila mwaka ni Siku ya Mitandao ya Kijamii duniani. Ni siku iliyoasisiwa mwaka 2010 na tovuti ya Mashable kwa lengo la kuenzi mchango mkubwa wa majukwaa ya kidigitali katika sekta ya mawasiliano.

Ikiwa ni miaka 16 tangu kuanzishwa kwa Siku hiyo, mitandao ya kijamii imepiga hatua kubwa, na sasa si tu mawasiliano, bali imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya binadamu.

ONGEZEKO LA WATUMIAJI

Ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2026 ya tovuti ya DataReportal Digital, watumiaji wa mitandao ya kijamii wamefikia bilioni 5.66, sawa na asilimia 68 ya watu wote duniani.

Ni tofauti na watumiaji bilioni 2.27 mwaka 2015, na wasiozidi milioni 500 mwaka 2005, huku kasi ya ongezeko hilo ikitokana na upatikanaji mkubwa wa mtandao, sambamba na wingi na unafuu wa bei wa simu-janja (smartphones).

Aidha, utafiti wa DataReportal imeonesha kuwa watumiaji wa kawaida hutumia saa 18 na dakika 36 kwa wiki wakiwa mitandaoni. Ni sawa na saa 2 na dakika 39 kila siku.

WAPI MATUMIZI NI MAKUBWA ZAIDI?

Wakati huo huo, mabara ya Asia, Ulaya na Amerika ya Kaskazini yametajwa kwenye ripoti hiyo kuwa ndiyo yenye matumizi makubwa zaidi ya mitandao ya kijamii.

Asia ya Mashariki inaongoza ikiwa na matumizi ya asilimia 88.1, ikifuatiwa na Ulaya ya Kaskazini (79%), Ulaya ya Magharibi (77.7%), na Amerika ya Kaskazini (74%).

Kwa Afrika, mgawanyo uko hivi; Afrika Magharibi (19%), Afrika Mashariki (12.1
6%) na Afrika ya Kati (12.1%).

MTANDAO UNAOONGOZA

Facebook inaongoza ikiwa na watumiaji 3.07 kwa mwezi. Mitandao mingine miwili ya Kampuni ya Meta – Instagram na WhatsApp, inashika nafasi ya pili kwa watumiaji bilioni 3 kila mmoja.

YouTube unaomilikiwa na Kampuni ya Google unashika nafasi ya tatu ukiwa na watumiaji bilioni 2.58 kwa mwezi, ukifuatiwa na TikTok (bilioni 1.99).

WATOTO WAPIGWA ‘STOP’

Kwa miezi ya hivi karibuni, mabunge ya nchi mbalimbali za Ulaya yamepaza sauti na hata kuwasilisha mapendekezo kwa serikali zao yakitaka watoto kuepushwa na matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuwalinda kimaadili na athari za kisaikolojia.

Desemba, 2025, Australia ikawa nchi ya kwanza kupiga marufuku matumizi ya mitandao kwa watoto wenye umri chini ya miaka 16.

Machi, 2026, Indonesia ikafuata nyayo na kuwa nchi ya kwanza barani Asia kufanya hivyo.

Wakati Brazil ikitaka mtoto mwenye umri chini ya miaka 16 kutumia mtandao kwa kuunganisha na mzazi au mlezi, Uturuki ilizuia kabisa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15.

Wiki chache zilizopita, ilikuwa ni zamu ya Uingereza, ambapo Sheria mpya itakayoanza mwaka 2027 inapiga marufuku watoto wenye umri wa miaka 16 kujihusisha na matumizi ya mitandao ya kijamii.

Related articles

Recent articles