TORONTO, Canada
BOSNIA and Herzegovina ni miongoni mwa timu zilizokata tiketi ya kucheza hatua inayofuata ya 32 Bora ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026).
Safari yao ya kuvuka makundi ilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Canada, kisha kufungwa mabao 4-1 na Uswis, kabla ya kuitandika Qatar mabao 3-1.
Katika hatua ya 32 Bora, Bosnia itaikabili Marekani, moja ya wenyeji watatu, ikishirikiana na Mexico na Canada. Mechi itachezwa Julai Mosi, 2026 mjini California.
DZEKO NDIYE SHUJAA WAO
Mashabiki wa soka nchini Bosnia wanamtambua straika wa zamani wa Manchester City, Edin Dzeko, kama shujaa wao, licha ya umri wake wa miaka 40.
Dzeko aliyewahi pia kutamba Ligi Kuu ya Italia (Serie A) akiwa na AS Roma, ndiye mchezaji mwenye mechi nyingi zaidi katika historia ya timu ya soka ya Taifa ya Bosnia.
Straika huyo amecheza michezo 150 akiwa na kikosi hicho, akimzidi 35 mchezaji anayeshika nafasi ya pili, Miralem Pjanic.
Wakati huo huo, Dzeko ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Bosnia, mabao 73, akimzidi 50 mshambuliaji anayeshika nafasi ya pili, Vedad Ibisevic.
“Anapokuwa uwanjani, matumaini yetu yanakuwa makubwa. Ana umri wa miaka 49 lakini yeye ni kama mwamvuli wa timu yetu. Naamini tupo naye kwa miaka michache ijayo, labda hadi wakati wa EURO,” anasema Ajdin Ljuca, mmoja ya mashabiki wa Bosnia.
“Ni kiongozi kweli kweli. Ni kama baba kwa chipukizi. Tunajivunia kuwa naye. Kwa vile anaelekea ukingoni mwa soka lake, ni vizuri kutumia mashindano haya kumshukuru Dzeko kwa yote,” anasema shabiki mwingine, Alim Djebo.
KOCHA HUYU HAPA
Katika benchi la ufundi, Bosnia wanaye Sergej Barbarez, kocha mwenye umri wa miaka 54, ambaye ni muumini wa mfumo wa 4-4-2.
Kwenye mechi zote tatu za msimu huu wa Kombe la Dunia, Barbarez aliamua kwenda na viungo wa ulinzi wawili (double pivot).
Ni kocha asiyetabirika katika upangaji wa kikosi. Katika mechi tatu, ni nyota watano pekee waliyocheza zote wakiwa ‘first eleven’.
Wachezaji hao ni kipa Nikola Vasilj, beki wa kushoto, Sead Kolasinac, kiungo wa ulinzi, Ivan Basic, straika wa Stuttgart, Ermedin Demirovic, na Esmir Bajraktarevic.
WATATOBOA KWA MAREKANI?
Mechi yao ya Julai Mosi, 2026 itakuwa mara ya nne kwa Bosnia kukutana ana kwa ana na Marekani. Timu hizo zimeshawahi kuvaana mara tatu.
Hata hivyo, mechi zote zilikuwa za kirafiki. Katika mchezo wa kwanza, Marekani ikiwa ugenini ilipata ushindi wa mabao 4-3.
Mechi mbili zilizofuata zilichezwa California. Moja ilikuwa ya suluhu (0-0) na nyingine ilimalizika kwa Marekani kushinda bao 1-0.
HISTORIA YAO KOMBE LA DUNIA
Hii ni mara ya pili kwa Bosnia kutia mguu kwenye fainali za Kombe la Dunia. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2014 lakini waliishia makundi.
Ni msimu ambao walifungwa mechi mbili za awali dhidi ya Argentina na Nigeria, kabla ya kuifunga Iran mabao 3-1 katika mchezo wa mwisho.


