27.3 C
New York

Israel, Marekani ‘zimechafua’ Uchaguzi Colombia?

Published:

BOGOTA, Colombia

RAIS aliyeondoka madarakani nchini Colombia, Gustavo Petro, ameendelea kutokuyatambua matokeo yaliyompa ushindi Abelardo de la Espriella.

De la Espriella (47), ameingia Ikulu akimpiku Ivan Cepeda katika Uchaguzi ulioanza Mei 31, 2026, na kurudiwa siku chache zilizopita baada ya ule wa awali kukosa mgombea aliyefikisha asilimia 50 ya kura.

Petro kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), amedai kuwa De la Espriella alisaidiwa na mataifa ya Israel na Marekani katika kunajisi taratibu za Uchaguzi.

Katika hatua nyingine, ameitaka Mahakama kuchunguza kilichotokea kwa kile alichokiita ‘uchafuzi’ wa mchakato wa kidemokrasia.

Mwanasiasa huyo alitaka kugombea muhula wake wa pili katika Uchaguzi huo lakini Mahakama ilimzuia kuingia kwenye kinyang’anyiro.

Katika madai yake, Petro amesema wageni (Marekani na Israel) walipewa nafasi ya kuingia kwenye tovuti ya Tume ya Uchaguzi na ‘kuchezea’ fomu iliyokuwa na idadi ya kura (E-14).

URAFIKI WAKE NA ISRAEL, MAREKANI

Kwa upande wake, De la Espriella, ambaye pia ana uraia wa Marekani, amekuwa hafichi sapoti yake kwa Israel, akiahidi mara kadhaa kuilinda jamii ya Wayahudi nchini kwake.

Hata baada ya kushinda kiti cha urais hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alimpongeza akisema:

“Nasubiri kwa hamu kushirikiana na wewe katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Israel na Colombia.”

Kwa upande wake, Rais Trump ameeleza kufurahishwa na ushindi wa De la Espriella, akisema:

“Alikuwa nafasi ya 10 (katika maoni ya wengi juu ya nafasi yake ya kushinda kiti cha urais). Nikamsapoti, akashinda. Alinipigia simu kunishukuru.”

Tofauti na De la Espriella, Petro ni mwanasiasa wa mrengo wa kushoto, hivyo amekuwa akitazamwa kwa jicho tofauti na serikali za Israel na Marekani.

Itakumbukwa, akiwa Rais, alisitisha ukaribu wa Colombia na Israel akieleza kutokukubaliana na kile kinachoendelea katika Ukanda wa Gaza dhidi ya raia wa Palestina.

Vilevile, Petro alijiweka mbali na sera za utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, hivyo kuchochea hasira za mataifa mawili hayo dhidi yake.

Pia, Petro alizuia ndege ya Marekani iliyokuwa imebeba wahamiaji kutua Colombia. Pia, aliitaka Marekani kuacha kuwachukulia kama wahalifu wahamiaji wa Colombia wanaoingia nchini humo.

Oktoba, 2025, Serikali ya Marekani ilimwekea vikwazo, kama ilivyofanya pia kwa familia yake, pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Colombia, ikiwahusisha na mtandao wa biashara za kulevya.

TAJIRI BILA UZOEFU WA SIASA

De La Espriella, ambaye ni msomi wa taaluma ya Sheria asiye na uzoefu wa kutosha katika siasa, anakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo Deni kubwa la Taifa.

Licha ya utajiri wake, taarifa za kiuchunguzi zilizoripotiwa na Gazeti la La Silla Vacia, zinadai kuwa bishara zake nyingi aidha zimekufa au ziko ‘ICU’ kutokana na madeni.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Gazeti hilo, biashara pekee ya faida kwake kwa sasa ni kampuni yake ya huduma za kisheria.

Suala la usalama, ambalo mtangulizi wake, Petro, alipiga hatua kubwa kwa kuanzisha mazungumzo na vikundi vya waasi, ni mzigo mzito mwingine anaotakiwa kuubeba De La Espriella.

Related articles

Recent articles