34.1 C
New York

Vocha za kukwangua kuanza kuondolewa mijini Julai 2026

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SERIKALI imepanga kuondoa matumizi ya vocha za kukwangua za muda wa maongezi katika maeneo ya mijini kuanzia Julai 1, 2026, hatua inayolenga kuharakisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika sekta ya mawasiliano na huduma za kifedha.

hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27, bungeni jijini Dodoma ambapo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeelekezwa kuendelea kusimamia mpango wa kuhamia kwenye matumizi ya njia za kidijitali katika ununuzi wa muda wa maongezi na vifurushi vya mawasiliano.

Kwa mujibu wa mpango huo, watumiaji wa simu katika maeneo ya mijini wataendelea kununua muda wa maongezi kupitia njia mbalimbali za kidijitali ikiwemo huduma za fedha kwa simu, programu za kampuni za simu na mifumo mingine ya kielektroniki.

Serikali inaeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za mawasiliano, kupunguza gharama za uchapishaji wa vocha pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali nchini.

Aidha, kuondolewa kwa vocha za kukwangua kunatarajiwa kupunguza matumizi ya karatasi na taka zinazotokana na vocha hizo, hatua inayochangia jitihada za uhifadhi wa mazingira.

Wadau wa sekta ya mawasiliano wanaeleza kuwa kwa sasa sehemu kubwa ya watumiaji wa simu tayari wanatumia njia za kidijitali kununua muda wa maongezi na vifurushi, jambo linalorahisisha utekelezaji wa mpango huo.

Hata hivyo, Serikali inatarajiwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya mifumo ya kidijitali ili kuhakikisha mabadiliko hayo hayaathiri upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa watumiaji.

Mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhamasisha uchumi wa kidijitali na kuongeza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Related articles

Recent articles