26.6 C
New York

Nini nyuma ya pazia ziara ya Xi Jinping nchini Korea Kaskazini?

Published:

PYONGYANG, Korea ya Kaskazini

RAIS wa China, Xi Jinping, yuko Korea ya Kaskazini kwa ziara ya siku mbili, Juni 8-9, 2026, ikilenga kutanua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya mataifa hayo ya barani Asia.

Hii ni ziara yake ya kwanza mjini Pyongyang kwa kipindi cha miaka saba lakini mwaka jana, 2025, Rais wa Korea ya Kaskazini, Kim Jong Un, alikuwa Beijing katika kumbukizi ya miaka 80 ya kumalizika kwa Vita kati ya China na Japan.

Safari hii, ziara ya Xi Jinping inakuja wakati huu Korea ya Kaskazini ikiwa imepiga hatua kubwa katika programu zake za utengenezaji wa silaha za kivita.

Je, nini kilichopo nyuma ya pazia katika ziara ya Rais Xi Jinping, ikikumbukwa kuwa ni mara yake ya kwanza tangu mwaka 2019. Makala haya yanachambua.

Ifahamike kuwa Rais Xi Jinping amepunguza kwa kiasi kikubwa safari zake za nje ya nchi. Na badala yake, viongozi wakubwa ndiyo wanaomfuata nchini kwake, kama walivyofanya Donald Trump na Vladimir Putin hivi karibuni.

Kuanzia mwaka 2013 hadi 2019, alikuwa na wastani wa safari 14 kwa mwaka. Idadi hiyo imepungua na kubaki wastani wa safari sita kwa mwaka (2022-2025).

Mwaka 2020, alikuwa na safari moja pekee ya nje ya nchi. Mwaka 2021, hakusafiri kabisa, wakati huo China ikiwa kitovu cha janga la Corona.

Ni kutokana na hilo, ziara ya Korea ya Kaskazini imeonekana kuwa na umuhimu mkubwa, kiasi cha Xi Jinping kuamua kufunga safari.

“Tukumbuke kuwa Xi Jinping hajasafiri sana nje ya nchi. Kwa Xi Jinping kuamua kwenda Pyongyang, inaonesha namna safari hiyo ilivyo na umuhimu mkubwa kwa China,” amesema mchambuzi wa siasa, William Yang.

Yang raia wa China, anasema moja ya sababu zinazoweza kuwa zimemvuta Xi Jinping kwenda ziara hiyo ni uhusiano mzuri na ulioimarika zaidi katika siku za hivi karibuni kati ya Korea ya Kaskazini na Urusi.

Kwa mingi, China na Korea ya Kaskazini zimekuwa na uhusiano mzuri si tu wa kidipmolasia, bali pia katika eneo la kiuchumi. Mathalan, biashara za Korea ya Kaskazini zinaitegemea China kwa asilimia 95.

Hata hivyo, China ina wasiwasi na uhusiano ulioanza na kushika kasi kati ya Korea ya Kaskazini na Urusi. Uhusiano ulioimarika tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka 2022.

Tangu kuanza kwa vita hivyo, Korea ya Kaskazini imekuwa ikiipatia silaha Urusi, teknolojia na hata wapiganaji. Tangu wakati huo, Urusi imeilipa Korea ya Kaskazini si chini ya Dola bilioni 14.4 kwa huduma hiyo.

Lee Sang Yong ni mwandishi wa habari, ambaye pia ni mtafiti mjini Seoul, Korea ya Kaskazini. Anasema China inahofia kupoteza ushawishi wake kwa Korea ya Kaskazini kutokana na uwepo wa Urusi.

“Beijing inataka kurejesha ushawishi wake kwa Korea ya Kaskazini na kuizuia isiitegemee sana Urusi,” amesema Lee akizungumzia ziara ya Xi Jinping.

Kwa mujibu wake, ziara ya Xi Jinping imelenga kwenda kuihakikishia Korea ya Kaskazini fursa za kiuchumi ili kuihamisha taratibu kutoka kwenye mikono ya Urusi.

Wakati huo huo, maendeleo ya tekonolojia ya utengenezaji wa silaha za kivita nchini Korea ya Kaskazini ni sababu nyingine ya ziara ya Xi Jinping.

Licha ya mataifa hayo kuwa na mkataba wa masuala ya kijeshi, China inahofia kasi kubwa ya Korea ya Kaskazini katika teknolojia, hasa inapokuwa inashirikiana na Urusi.

Hivi karibuni, Rais wa Korea ya Kaskazini, Kim, alifanya ziara katika kiwanda kipya cha uzalishaji wa silaha za nyuklia. Hii inaipa hofu China, kwamba huenda inapoteza ushawishi wake wa kijeshi barani Asia.

Related articles

Recent articles