LONDON, Uingereza
AMEKIRI mara kadhaa kuwa ipo siku atarejea kwenye kazi ya ukocha. Kwa sasa, Jurgen Klopp ni Mkuu wa Maendeleo ya Soka wa Kampuni ya Red Bull.
Taasisi hiyo inayomiliki klabu za soka, zikiwamo Leeds United ya England na RB Leipzig ya Bundesliga, ilimpa ajira hiyo Januari, 2025.
Taarifa zinaeleza kuwa Mjerumani huyo atajiuzulu hivi karibuni. Je, ataibukia wapi endapo atarudi kwenye ukocha?
Liverpool
Alifanya kazi miaka tisa katika klabu hiyo yenye masikani yake mjini Merseyside. Akiwa Anfield, aliipa Liverpool mataji ya Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya katika mechi 489.
Wakati huu Liverpool ikihusishwa na mpango wa kumtimua Arne Slot, Klopp anaweza kuwa mtu sahihi wa kupewa kijiti.
Oktoba, 2025, aliweka wazi ndoto yake ya kurudi Anfield akisema: “Kama nitarudi (kwenye ukocha), lazima itakuwa Liverpool.”
Borussia Dortmund
Aliwahi kufanya kazi katika klabu hiyo ya Bundesliga. Kama ilivyo kwa Liverpool, Klopp ana heshima kubwa pale Dortmund.
Aliinoa timu hiyo kuanzia mwaka 2008 hadi 2015. Atakumbukwa kwa kuipa mataji mawili ya Ligi Kuu (Bundesliga); 2011 na 2012.
Pia, mashabiki wa Dortmund hawajasahau kuwa Klopp aliipeleka timu hiyo hadi fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa sasa, Dortmund iko chini ya kocha Niko Kovac aliyeajiriwa mwaka 2025. Kwa mwenendo wa timu hiyo, huenda huu ukawa msimu wake wa mwisho.
Atletico Madrid
Zipo taarifa kuwa Klopp anavutiwa na mpango wa kuchukua mikoba endapo Diego Simeone ataliacha benchi la ufundi mwishoni mwa msimu huu.
Simeone anahusishwa na klabu za Italia na inaelezwa kuwa mabosi wa Atletico wameanza kuwasiliana na Klopp.
Real Madrid
Wababe hao wa jijini Madrid wananolewa na kocha wa muda, Alvaro Arbeloa, na dalili zinaonesha kuwa ataondoka mwishoni mwa msimu huu.
Mabosi wa Madrid hawajawahi kuficha mapenzi yao kwa Klopp. Walijaribu kumuajiri hata alipoondoka Liverpool.
Kwa sasa, hakuna mazungumzo yaliyofanyika kati yake na Madrid lakini haitashangaza kuona kocha huyo akiwa Santiago Bernabeu msimu ujao.


