20.4 C
New York

Infographic| Duterte; Rais asiyeishiwa vituko anayewindwa na ICC

Published:

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inaendesha upelelezi dhidi ya Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, juu ya madai ya mauaji aliyotekeleza katika operesheni yake ya kutomokeza biashara ya dawa za kulevya nchini humo.

Kile kilichoelezwa na ICC ni kwamba watu takribani 6,000 wameuawa katika operesheni za Rais Duterte. Aidha, waendesha mashitaka wa Mahakama hiyo wanasema wapo mashahidi 200 wanaothibitisha namna kiongozi huyo alivyotekeleza uhalifu huo.

Hata hivyo, tayari mwanasheria wa Rais Duterte ameshasema ICC haitaruhusiwa kuingia Ufilipino kwa ajili ya kukusanya ushahidi. Kwa mujibu wa mwanasheria, Ufilipino ilishajitoa ICC, hivyo taasisi hiyo haiwezi kuingilia chochote kinachofanywa na Rais Duterte.

Kufikia sasa, ICC iliyoanza kufanya kazi mwaka 2002, imeshawahi kuwatia mkononi viongozi 45; Omar al-Bashir (Sudan), Uhuru Kenyatta (Kenya), Muammar Gaddafi (Libyan), Laurent Gbagbo (Ivory Coast), kwa kuwataja kwa uchache.

Duterte ni nani?

Alizaliwa mwaka 1945 na anatokea familia ya siasa kwani baba yake aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za Serikali, ikiwamo ya meya. Duterte ambaye ni msomi wa sheria, alichaguliwa kuwa meya wa Davao mwaka 1988. Kutokana na mafanikio yake ya kupunguza uhalifu na vitendo vya rushwa akiwa Davao, haikushangaza kuona akikusanya kura milioni 16 (39%) zilizompa urais wa Ufilipino mwaka 2016.

Katika ndoa yake ya kwanza, Duterte ambaye wazazi wake wameshafariki, alimuoa muhudumu wa ndege aitwaye Elizabeth Abellana Zimmerman. Walibahatika kupata watoto watatu, kabla ya kuachana na Zimmerman.

Akizungumzia kuvunjika kwa ndoa yao iliyodumu miaka 27, Zimmerman aliyefariki kwa saratani ya matiti mwaka 2015 alisema Duterte ni kiongozi mzuri lakini awapo nyumbani huwa hana muda wa kubembeleza kwenye mapenzi.

Baadaye, Duterte alimuoa Cielito Avancena na kwa sasa wawili hao ni wazazi wa mtoto wa kike aitwaye Veronica. Aidha, Duterte ni babu wa wajukuu nane waliogawanyika katika Dini kubwa mbili; wanne ni Waislam na wengine ni Wakiristo.

Unazijua kauli, matukio yake tata?

Mwaka 1989, Duterte akiwa meya wa Jiji la Davao, aliwashangaza wengi kwa kitendo chake cha kuleta utani juu ya tukio la mwandishi wa habari wa kike kubakwa wakati wa mgomo uliotokea gerezani. Akizungumzia tukio hilo, Duterte alitania kwa kusema yeye kama meya alitakiwa kuwa wa kwanza ‘kumuonja’ mrembo huyo, kabla ya wale waliombaka.

Mwaka 2015, akiendelea kushikilia wadhifa wa meya, Duterte alimwita Papa Francis kuwa ni ‘mtoto wa malaya’. Tusi hilo analopenda kulitumia mara nyingi (hata dhidi ya Barack Obama) lilimfikia Papa baada ya Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani kusababisha foleni kubwa alipotembelea Jiji la Manila. Mwaka huo pia, Duterte akawa gumzo tena, safari hii akisema ana wake wawili na ‘michepuko’ miwili.

Taasisi mbalimbali za kupigania haki za binadamu zinadai Duterte aliratibu mauaji ya watu zaidi ya 1,400 akiwa Meya wa Jiji la Davao. Mauaji hayo yalifanyika kuanzia mwaka 1998 hadi 2016. Kwa mwaka 2019 pekee, utawala wake uliua watu 5,100 waliotajwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Akiwa kwenye kampeni mwaka 2016, Duterte alikiri mbele ya umati kuwa anapenda kuua kwa kutumia bastola, akisimulia alivyowahi kutumia silaha hiyo kukata maisha ya mwanafunzi mwenzake wa chuo aliyekuwa anamtania.

Ukiachana na hiyo ya mwaka 2016, kauli yake tata nyingine ni ile ya mwaka juzi akiwa kwenye mkutano wa hadhara, ambapo Duterte alisema aliwahi kuwa ‘shoga’ lakini alijitibu na kuachana kabisa na tabia chafu hiyo.

Kwani Wafilipino wanasemaje?

Licha ya utawala wake kunyooshewa kidole na jumuhiya za kimataifa, raia wa Ufilipino hawaonekani kuwa na shida naye. Kwa utafiti wa mwaka juzi, asilimia 79 ya wananchi walieleza kumkubali. Wengi (92%) walivutiwa pia na namna Duterte alivyopambana na Corona, njia kubwa aliyoitumia ikiwa ni ‘kuwafungia ndani’ raia wake.

Je, imani kubwa hiyo ya wananchi kwa Duterte itamrejesha madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwakani? Na je, endapo atashinda, wakosoaji wake watakuwa na la kumnyooshea kidole ikiwa raia wameamua aendelee kuwaongoza?

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img