Na Imani Nathaniel, Gazetini
MKURUGENZI Mashitaka nchini (DPP), amewafutia kesi washtakiwa wawili kati ya sita waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia.
Waliofutiwa mashtaka na kuachiwa huru ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo Zenabu Islam(61) ambaye ni mkazi wa Kariakoo na mshtakiwa wa tatu, Ashour Awadh Ashour(38) mkazi wa Ilala.
Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Godfrey Mhini.


Wamefutiwa mashtaka yao baada ya upande wa Jamhuri kuieleza mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.
Awali, wakili wa Serikali Christopher Olembelle akisaidiana na Neema Kibodya, aliileleza Mahakama hiyo kuwa DPP amewasilisha hati ya kutokuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa wawili, chini ya kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023.
Wakati washtakiwa hao wawili wakifutiwa mashtaka yao, wenzao wanne bado wanaendelea na kesi hiyo ambao ni Leondela Mdete(49) Soster Nziku(55) Aloyce Sangawe(59) Stephen Nziku(28) wote ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Novemba 16, 2025 katika mtaa wa Mchikichi na Congo eneo Kariakoo, washtakiwa isivyohalali walishindwa kutumiza majukumu yao na kusababisha vifo vya watu 31.


