3.9 C
New York

Yanga, Injinia Hersi; ‘win-win situation’ iliyorudisha chenji

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

‘Win-win situation’ ni nini? Ni pale pande mbili au zaidi zilizo kwenye mahusiano au ushirika wa kibiashara zinaponufaika kwa pamoja, pasi na kuwapo kwa hisia za kuumizana.

Katika dhana hii, hakupaswi kuwapo na upande unaoumia, huku mwingine ukinufaika zaidi. Kila upande unufaike na kufurahia uwepo wake kwenye ushirika.

Tuje kwa Yanga na Injinia Hersi. Uhusiano/ushirika wao unaotokana na nafasi aliyonayo katika klabu hiyo. Nafasi ya Rais wa Yanga.

Tangu Injinia Hersi alipoingia Yanga na kushika nafasi hiyo, pande mbili hizo zimekuwa na kile nilichotangulia kukisema, yaani ‘win-win situation’.

Tujikumbushe; Injinia Hersi aliikuta Yanga katika hali mbaya si tu ndani, bali hata nje ya uwanja. Wanayanga wanakumbuka vizuri.

Yanga ambayo ndani ya uwanja haikuwa imetwaa taji la Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo. Simba ilibeba mara zote hizo.

Yanga ambayo ushiriki wake kwenye michuano ya kimatafa haukutofautiana na usindikizaji. Haikuwa rahisi hata kuvuka hatua ya makundi.

Nje ya uwanja, ilikuwa ni Yanga ‘inayonuka njaa’. Ilishuhudiwa mara kadhaa ikitembeza bakuli majukwaani wakati mechi ikiendelea. Yanga ilifikia hapo!

Ni kutokana na hali mbaya ya uchumi, klabu hiyo chini ya Mwenyekiti Mshindo Msolla, ikaja na wazo lililoonekana la kibunifu. Unaikumbuka ‘Kubwa Kuliko’?

Haikutofautiana sana kutembeza bakuli, ingawa hii ilikuwa ya kisasa zaidi, ikikutanisha wanachama na wadau wazito walioingia mifukoni na kuchangia fedha za kuisaidia Yanga.

Huko ndiko shimoni ilikokuwa Yanga. Shimo lenye kila aina ya dhiki pasipo faraja na fedheha za ndani na nje ya uwanja. Baada ya Injinia Hersi kuwa rais, mambo yamebadilika ghafla sana. Hatusikii tena kuhusu kutembeza bakuli viwanjani.

Pia, Kubwa Kuliko, ambayo ilionekana kuwa ni ubunifu wakati wa njaa kali, nayo imeota mbawa kwa kasi ya upepo wa kisukisuli.

Chini ya uongozi wa Injinia Hersi, Yanga sasa inapima uwezo wa wa kocha inayemuajiri kupitia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Kufika hatua ya makundi siyo shida zao tena!

Wakati huo huo, haiwi kwa Yanga pekee kunufaika na ushirikiano wake na Injinia Hersi. Naye kwa namna moja au nyingine, ananufaika na ‘kuinjoi’ ukaribu wake na Yanga. Kivipi?

Kwa kipindi chake cha uongozi, Injinia Hersi ameweza kupiga hatua kubwa katika mafanikio binafsi ndani ya mchezo wa soka.

Leo hii, kupitia ushirikiano wake na Yanga, Injinia Hersi ni Rais wa Klabu za soka zilizo chini ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

Kama hiyo haitoshi kuonesha ukubwa aliofikia kwenye soka, hivi karibuni aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Mafanikio ambayo kama si kufanya kazi na klabu yenye historia kubwa na ushawishi wa kutosha ndani na nje ya nchi, huenda angeyakosa au angechelewa mno kuyafikia.

Hiyo ndiyo ‘win-win situation’. Wakati Yanga wakijivunia makubwa aliyowafanyia Injinia Hersi, naye kwa upande wake anaiona klabu hiyo ikiwa imempandisha ‘fasta’ kwenye kilele cha mafanikio binafsi ndani ya soka la ndani na nje ya Afrika.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img