Na Imani Nathaniel, Gazetini
SHAURI la kuporomoka kwa ghorofa la Kariakoo limekwama kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo kwa washitakiwa wa kesi ya mauaji bila kukusudia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na upande wa Jamhuri kutokana na baadhi ya nyaraka kubainika hazipo kwenye mfumo wa mahakama.
Wakili wa serikali Glory Kilawe, ameeleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam , mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini.
Wakili huyo amedai, kesi imeletwa kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo, lakini baada ya kupitia jarada halisi na taarifa iliyopandishwa katika mfumo wa mahakama, wamebaini baadhi ya nyaraka hazipo.

Kutokana na hali hiyo, ameomba mahakama ipange tarehe nyingine, wafanye marekebisho. Hakimu alikubali ombi hilo na kupangiwa Desemba 30, 2025.
Kesi hiyo inawakabili wafanyabiashara sita ambao ni Lendela Mdete, Mkazi wa Mbezi , Zenabu Islam maarufu kama Zaibanu, mkazi wa Kariakoo na Ashour Ashour mkazi wa Ilala.
Wengine ni Soster Nziku mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe mkazi wa Sinza na Stephen Nziku mkazi wa Mbezi beach.
Katika kesi hiyo ilielezwa upande wa jamhuri unatarajiwa kuwa na mashahidi 55 na vielelezo 54 kesi itakapoanza kusikilizwa.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 16, 2024 Mtaa wa Mchikichi na Kongo, Kariakoo ,jijini Dar es Salaam.
Ilidaiwa kwamba, washitakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha vifo vya watu 31 ambao ni Said Juma, Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu, na Chatherine Mbilinyi.
Wengine ni Elton Ndyamkama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuf, Ally Omary, Ajuae Iyambilo, Mary Lema, Khatolo Juma, Sabas Swai, Pascal Ndungulu, Brighette Mbembele, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Issa Bakari, Lulu Sanga, Happnees Malya na Brown Kabovera.


