HARARE, Zimbabwe
MAMLAKA nchini Afrika Kusini zimemshikilia na kumuhukumu kifungo cha miaka mitano gerezani raia mmoja wa Zimbabwe aliyekuwa safarini akielekea kwenye vita kati ya Ukraine na Urusi.
Afrika Kusini ina sheria kali zinazowazuia raia wake na wa kigeni waliopo nchini humo kujihusisha na vita vya nje.
Wesley Sothole, kijana mwenye umri wa miaka 24, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani na kuamriwa kuondoka Afrika Kusini.
Taarifa zinaeleza kuwa Sothole alikuwa mmoja ya Wazimbabwe watano waliokamatwa wakiwa Uwanja wa Ndege wa OR Tambo mjini Johannesburg.
Hata hivyo, waendesha mashitaka wa Afrika Kusini hawajaeleza ni upande upi kati ya Ukraine na Urusi uliowahitaji raia hao wa Zimbabwe.


