MUNICH, Ujerumani
KUFIKIA mwaka 2045, nchi ya Ujerumani itakuwa kwenye uhaba mkubwa wa wafanyakazi kwa kuwa idadi kubwa ya raia wake watakuwa wazee, kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Idadi ya Watu na Maendeleo ya jijini Berlin.
Kwa mujibu wa utafiti huo, idadi ya watu nchini Ujerumani inatarajiwa kupungua kutoka milioni 83.5 mwaka 2025 hadi milioni milioni 81.8 ifikapo mwaka 2045.
Utafiti umeeleza pia, kwamba changamoto iliyopo nchini humo kwa sasa ni idadi kubwa ya wastaafu, ikilinganishwa na vijana wanaoingia kwenye soko la ajira.
Ni kutokana na mazingira hayo, utafiti umeeleza kuwa idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi inatarajiwa kupungua kwa asilimia 4.7 kufikia mwaka 2045.
Akizungumzia matokeo ya utafiti, Rais wa Taasisi hiyo, Catherina Hinz, amesema hali inakuwa mbaya zaidi kutokana na kupungua kwa kasi ya kuzaliana.
Takwimu mbalimbali zimeonesha kuwa katika miji mingi, ikiwamo Berlin na Munich, idadi ya vifo kwa mwaka ni kubwa kuliko ile ya watoto wanaozaliwa.


