10.4 C
New York

Ulevi wa pombe unavyomaliza vijana Kilimanjaro

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini – KILIMANJARO

VIJANA zaidi ya 15 wanadaiwa kufariki ndani ya siku 10 katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, huku matumizi ya pombe kupita kiasi yakitajwa kuwa miongoni mwa sababu.

Madai hayo yametolewa na Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi, Novemba 17, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Old Moshi Mashariki wilayani Moshi katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.

Makoi alisema tangu arejee kutoka Bungeni Novemba 7 hadi siku hiyo ya mkutano, amehudhuria mazishi ya vijana zaidi ya 15, huku chanzo cha vifo hivyo ikidaiwa kuwa ni ulevi kupita kiasi.

Akieleza sababu za wasiwasi wake, Makoi alisema baadhi ya wafanyabiashara wanauza pombe kali ndani ya maduka, licha ya leseni zao kutoruhusu biashara hiyo.

Alisema hali hiyo inachangia madhara kwa vijana na kuwataka wanaouza pombe kali aina ya gongo kupunguza, kama si kuacha kabisa, biashara hiyo.

Kwa upande wake, Babu alisema matumizi ya mirungi pia ni changamoto katika eneo hilo, akieleza kuwa operesheni za polisi zimefanikisha kukamata pikipiki 10 zinazodaiwa kutumika kusafirisha kilevi hicho.

Wakati huo huo, aliagiza maofisa biashara na viongozi wa halmashauri kukagua maduka yanayouza pombe kinyume na masharti ya leseni na kuwachukulia hatua wanaokiuka sheria.

Babu aliwataka wazazi na wazee kushiriki katika kuwaelekeza vijana kuepuka ulevi na kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, akisema eneo hilo lina ardhi nzuri inayoweza kutumika kwa kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi.

Related articles

Recent articles