5.9 C
New York

Dk. Mwigulu kuzindua kitambulisho cha taifa kilichoboreshwa Pwani

Published:

Na Gustaphu Haule, Gazetini- PWANI

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Pwani kuanzia Novemba 18, 2026, ambapo atazindua Kitambulisho cha Taifa kilichoboreshwa pamoja na huduma mpya za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ametoa taarifa hiyo Novemba 17, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi mdogo wa mikutano uliopo katika jengo la ofisi yake.

Amesema Waziri Mkuu atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika uzinduzi huo utakaofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani ya Mailimoja, Kibaha.

Nyongo amesema baada ya uzinduzi huo, Waziri Mkuu atafanya mkutano wa hadhara na kuzungumza na wananchi wa Manispaa ya Kibaha.

“Tunajivunia heshima hii ya Mkoa wa Pwani kuwa mwenyeji wa uzinduzi huu ambao una umuhimu mkubwa katika kuendeleza mfumo wa utambulisho wa wananchi na kuboresha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma nchini,” amesema Nyongo.

Ameeleza kuwa uzinduzi huo si tukio la kutambulisha kitambulisho kilichoboreshwa pekee, bali ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa utambulisho wa Taifa, kuongeza ufanisi katika utambuzi wa watu, kulinda usalama wa taarifa za wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazohitaji utambulisho rasmi.

Aidha, amesema sambamba na uzinduzi wa Kitambulisho cha Taifa kilichoboreshwa, toleo la mwaka 2026, NIDA itazindua huduma mpya ijulikanayo kama *Huduma Bila Foleni*, inayolenga kupunguza muda wa wananchi kusubiri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Amesema jambo la kipekee katika uzinduzi huo ni fursa kwa wananchi kupata huduma moja kwa moja katika eneo la tukio, huku huduma hizo zikilenga wananchi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Pwani.

Nyongo ametaja huduma zitakazotolewa kuwa ni usajili wa wananchi ambao bado hawajasajiliwa katika mfumo wa NIDA, uhakiki na marekebisho ya taarifa za utambulisho, pamoja na kutoa elimu na ushauri kuhusu taratibu na huduma mbalimbali za mamlaka hiyo.

Huduma nyingine ni ufuatiliaji wa hatua na hali ya maombi ya Vitambulisho vya Taifa, pamoja na ugawaji wa vitambulisho vilivyokamilika kwa wananchi wenye namba za utambulisho wa Taifa ambao bado hawajavichukua.

Amesema uzinduzi huo ni fursa kwa wananchi kupata taarifa, kutatua changamoto zinazohusu utambulisho wao na kunufaika na huduma za NIDA bila kusubiri fursa nyingine.

Kutokana na umuhimu wa tukio hilo, Nyongo amewataka wananchi wote wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi kushiriki uzinduzi huo, kutumia huduma zitakazotolewa na NIDA na kupata nafasi ya kumsikiliza Waziri Mkuu.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Kibaha, akiwemo Waziri Manyakala, wameeleza kufurahishwa na ujio wa Waziri Mkuu, wakisema wanatarajia kutumia fursa hiyo kuwasilisha changamoto zinazowakabili, zikiwemo za miundombinu ya barabara.

Related articles

Recent articles