5.9 C
New York

Koffi Olomide: Skendo ya Ukimwi, ugomvi wake na Papa Wemba – [3]

Published:

KINSHASA, DRC

MWANZONI mwa mwaka 1987, wakati huo Koffi akiwa kwenye kilele cha mafanikio, alikwaa skendo nzito akidaiwa kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi akiwa barani Ulaya.

Kwa kiasi kikubwa, kashfa hiyo ilimtesa vilivyo, kiasi cha kulazimika kuandika ngoma kadhaa za kujitetea, zikiwamo ‘Ngulupa’, ambayo ndani yake anasikika akisema ‘Bomoni te, boyoki yango, tika kotuba koloba’, yaani ‘hakuna ulichoona, unasikia tu; acha kuzungumzia usiyoyajua’.

Pia, katika hilo hilo la skendo yake ya Ukimwi, aliandika wimbo mwingine uitwao ‘Dieu Voit Tout’, ambao ndani yake anasema ‘Kuna na mboka lola ata bato oyo ya sida, bazuaka pe kimia oyo ya seko’, yaani ‘walau wenye Ukimwi hawajasahaulika mbinguni’.

Katikati ya miaka ya 1987, Koffi aliachia albamu yake ya tano, ‘Rue D’Amour’, iliyokuwa na ngoma kali za mapenzi zilizofanya vizuri, ikiwamo ‘Stephie’.

Pia, katika alitumia albamu hiyo kuwapiga madongo wapinzani wake kupitia nyimbo ‘Petit frere ya Jesus’ na ‘Droits de l’homme’.

Baada ya ‘Henriquet’ ya mwaka 1988, Koffi aliachia albamu ya saba, ‘Elle et Moi’, mwaka 1989, na ya nane ‘Les prisonniers dorment’ iliyouza nakala zaidi ya 100,000 duniani kote.

Mafanikio hayo yalifuatiwa na albamu mbili za Bendi yake ya Quartier Latin, ‘Pas de faux pas’ [1992] na ‘Magie’ [1994], ambazo baadhi ya video zake zilirekodiwa Marekani na Ufaransa.

Nini chanzo cha ugomvi wake na Papa Wemba? Kama ilivyoelezwa katika moja ya sehemu zilizopita za makala haya, Koffi na Papa Wemba waliwahi kuwa washikaji na hata kushirikiana na baadhi ya nyimbo.

Ndiyo, katika miaka ya 1970, wakati huo Koffi akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Bordeaux, Papa Wemba alikuwa akimkubali na hata kumpachika jina la ‘L’Homme a idee [Mtu mwenye akili kubwa].

Tukaona pia, kwamba wakati Koffi alipokuwa akirejea DRC kwa likizo ya masomo, alikuwa akifanya kazi na Bendi ya Papa Wemba iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Viva La Musica. Zipo tetesi pia, kwamba Koffi alikuwa akimwandikia nyimbo Papa Wemba wakati huo.

Hata hivyo, vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa ugomvi wao wa magwiji hao ulianza mwaka 1993 na chanzo kikubwa ni mapenzi. Kwamba Papa Wemba alianzisha uhusiano wa kimapenzi na mmoja ya madansa wa Koffi aitwaye Rosette Kamono.

Katika kujibu mapigo, Koffi naye alitoka kimapenzi na mmoja ya wasichana waliokuwa kwenye mahusiano na Papa Wemba, hali iliyosababisha uhasama mkubwa kati ya wanamuziki hao.

Aidha, vyanzo vingine vya habari vinamtaja mtunzi wa muziki, Felix Wazekwa, kuwa ndiye chanzo cha bifu kati ya Koffi na Papa Wemba.

Wazekwa alikuwa Rafiki mkubwa wa Koffi na alimsaidia kwa kiasi kikubwa wakati mwanamuziki huyo anaandaa albamu yake ya ‘Noblesse Oblige’ iliyoingia sokoni na kufanya vizuri mwaka 1993.

Koffi alikasirika baada ya kuona Wazekwa ameshirikiana na Papa Wemba kuandaa albamu kubwa mbili, ‘Foridoles’ (1994) na ‘Pole Position’ (1996), ambazo ziliweza kumrudisha kwenye chati Papa Wemba.

Itaendelea …

Related articles

Recent articles