10.6 C
New York

Huyu ndiye paka mzee zaidi duniani

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

AKIWA na umri wa miaka 31, Millie anatajwa kuwa ndiye paka mzee zaidi duniani. Leslie Greenhough, mkazi wa jijini Manchester mwenye miaka 71, ndiye anayemmiki mnyama huyo.

Awali, kwa mujibu wa Leslie, paka huyo alikuwa akimilikiwa na mkewe, Paula, ambaye naye alianza kumfuga tangu akiwa na umri wa miezi mitatu.

Leslie anasema amekuwa akiitunza afya ya paka wake huyo kwa umakini mkubwa, ikiwa ni pamoja na kumpatia aina nzuri ya vyakula, ikiwamo samaki.

Kama hiyo haitoshi, paka huyo amekuwa akinywa maji safi yanayouzwa dukani, achilia mbali kutengewa sofa maalumu kwa ajili ya kujipumzisha.

Tofauti na paka wengine, Millie amekuwa akifanywa sherehe za kila inapofika siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake [birthday]. ‘Bosi’ wake humuwekea bakuli alilojaza nyama ya kuku ili kumfanya aifurahie siku hiyo.

Mathalan, wakati Millie anatimiza miaka 30, Leslie aliamua kumnunulia keki, ambayo ilipambwa kwa picha ya uso wake. Pia, Leslie alinunua mishumaa 30 siku hiyo.

Kipindi hiki joto likiwa limepanda kwa kiasi kikubwa nchini Uingereza, Leslie ametenga feni mbili, maalumu kwa ajili ya kumsaidia Millie kukabiliana na hali hiyo.

Leslie na Paula walikutana mwaka 2012, kabla ya kufunga ndoa Siku ya Wapendanao [Valentine’s Day] ya mwaka 2014.

Akimzungumzia Millie, Leslie anasema: “Kwa miaka mingi, Millie alikuwa akiteswa na paka wenzake huko nje, hivyo alianza kubaki ndani.”

Paula alifariki mwaka 2020 kutokana na ugonjwa wa Corona. Leslie anasema Millie aliumizwa na kifo cha Paula, kiasi cha kutokula vizuri.

“Nafikiri Millie alijua kabisa kwamba mke wangu alikuwa mgonjwa,” anasema Leslie na kuongeza: “Millie hakula chochote [siku ya kifo cha Paula].”

Leslie anasema ndoto yake ni kuona Millie anaingia kwenye rekodi za Guinness Book of Records na kutambulika kama paka mwenye umri mkubwa zaidi duniani lakini changamoto ni kukosekana kwa ushahidi.

“Isivyo bahati, mtu pekee anayeweza kuthibitisha juu ya umri wa Millie ni mke wangu,” anasema Leslie na kuongeza kuwa ushahidi pekee alionao kwa sasa ni picha ya paka huyo ya mwaka 1995.

Hata hivyo, Leslie anasema mwonekano wa sasa wa Millie umebadilika, tofauti na alivyokuwa mwaka 1995, hivyo bado ni ngumu kuithibitishia Guinness Book of Records.

Related articles

Recent articles