3.4 C
New York

Wivu wa mapenzi usiwe sababu ya mauaji-Serikali

Published:

Na Mwandishi wetu, Gazetini-Njombe

SERIKALI imetoa onyo kwa wanaume nchini dhidi ya kuruhusu wivu wa kimapenzi kuwachochea kufanya vitendo vya ukatili na mauaji, akisisitiza kuwa wanaojihusisha na uhalifu huo watachukuliwa hatua za kisheria.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi jana Oktoba 17, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe, katika mkutano wa Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi.

Amesema migogoro ya kimapenzi imekuwa chanzo cha vitendo vya ukatili na mauaji katika baadhi ya mahusiano, hivyo kuwataka wanaume kudhibiti hisia zao na kuepuka maamuzi yanayoweza kuhatarisha maisha ya wengine na kuwaingiza matatani kisheria.

“Wivu wa mapenzi, watu wanauana sana. Lazima ujue unapoingia kwenye mahusiano ya mapenzi, mapenzi haya ni ya biashara, ni ya mkopo, ya upendo au ni mapenzi ya mazingira, lazima ujue,” amesema Katambi.

Ameeleza kuwa baadhi ya wanaume hutumia fedha nyingi kuwahudumia wenza wao, lakini hujikuta katika migogoro wanapohisi kuwa wenza wao wamewaacha au kuanzisha mahusiano na watu wengine.

Amesisitiza kuwa hali hiyo haipaswi kuwa sababu ya kufanya uhalifu, akiwataka wanaume kutafakari kwa kina kuhusu mahusiano yao na kutafuta njia salama za kutatua migogoro.

“Lazima tutafakari, kwa sababu mapenzi yanapelekea mauaji, Mheshimiwa Makamu wa Rais. Mtu anampenda mtu kumbe anampenda kwa pesa, wewe unampenda kwa moyo. Wanaume angalieni sehemu za kuweka mioyo yenu. Huo ni ujumbe wangu, msije mkaingia kwenye jinai, mwishowe utaua, utaishia jela na watu watateseka,” amesema.

Aidha, Katambi amewataka wanaume kuwa makini katika mahusiano yao na kuhakikisha kuwa wivu wa kimapenzi hauwapelekei kufanya vitendo vya uhalifu, akisisitiza umuhimu wa kudhibiti hisia na kutanguliza usalama wa kila mmoja.

Related articles

Recent articles