Na mwandishi wetu, Gazetini
JUMLA ya watahiniwa 667,040 wanatarajiwa kuanza kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2026, utakaofanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6 katika shule za sekondari 6,265 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea nchini.
Kati ya watahiniwa hao, 644,085 ni watahiniwa wa shule, huku 22,955 wakiwa watahiniwa wa kujitegemea.
Akizungumza leo, Oktoba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema kati ya watahiniwa wa shule, wavulana ni 297,309, sawa na asilimia 46.16, huku wasichana wakiwa 346,776, sawa na asilimia 53.84.
Amesema kati ya watahiniwa wa shule, 910 wana mahitaji maalum. Kati yao, 455 wana uoni hafifu, 13 hawaoni, 98 wana uziwi, 21 wana ulemavu wa akili na 323 wana ulemavu wa viungo.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, Profesa Mohamed amesema wavulana ni 10,223, sawa na asilimia 44.53, huku wasichana wakiwa 12,732, sawa na asilimia 55.47.
Aidha, amesema watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalum ni 73, ambapo 69 wana uoni hafifu na wanne hawaoni.
Profesa Mohamed ameongeza kuwa mwaka 2025, jumla ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa 569,883. Hivyo, mwaka 2026 kumekuwa na ongezeko la watahiniwa 74,202, sawa na asilimia 13.02, ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Baraza la Mitihani la Tanzania limetoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia mtihani huo kutekeleza majukumu yao kwa umakini, uadilifu na kuzingatia taratibu zote za usimamizi wa mitihani.


