22.8 C
New York

Akutwa hana hatia akisubiri kifo gerezani

Published:

LOS ANGELES, Marekani

DOUGLAS Stewart Carter mwenye umri wa miaka 71, amerejea uraiani baada ya kuachiwa kwa dhamana. Ni baada ya miaka 41 ya kusota gerezani ndipo waendesha mashitaka walipobaini kuwa hakuhusika katika mauaji ya mwanamke aitwaye Eva Olesen.

Tangu alipohukumiwa kifo, Douglas amekuwa akisisitiza kuwa hana kosa na mwaka jana [2025], ndipo Mahakama Kuu ya Utah ilipoagiza kuanza upya usikilizaji wa kesi baada ya kutilia shaka namna uchunguzi ulivyofanyika.

Ilikuwa hivi; Februari, 1985, Olesen ambaye ni shangazi wa mmoja ya wakuu wa polisi mjini Utah, aliuawa baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali, kisha kupigwa risasi ya kichwa.

Wakati huo, Douglas ambaye ni mkazi wa Chicago alikuwa akiishi kwa mama yake mjini Utah. Polisi walimshuku kuhusika na mauaji kwa maelezo kwamba alikuwa akijaribu kupora.

Kwa hofu aliyokuwa nayo, Douglas aliamua kuondoka Utah lakini aliishia mikononi mwa polisi akiwa Nashville, Tennessee. Alipokamatwa, alisaini fomu ya kukiri kosa, ingawa baadaye aliiambia mahakama kuwa alilazimika kukiri baada ya mateso makali aliyopewa na polisi.

Baadaye, mashahidi wawili walifika mahakamani kuthibitisha kuwa alihusika, ingawa baadaye [2011] walisema waliidanganya mahakama baada ya kupewa rushwa na polisi.

Kwa mujibu wa mashahidi hao, mbali na rushwa, pia walitishiwa na polisi hao wakiambiwa wangekamatwa na kubambikiwa kesi endapo wangekataa kwenda mahakamani ‘kumkaanga’ Douglas.

Mwaka jana, miaka 41 tangu hukumu ya kifo iliposomwa, mahakama iliagiza kesi kusikiliwa upya. Katika ushahidi mpya, ilibainika kuwa kisu kilichotumika kumdhuru Olesen ni cha jikoni kwake.

Kama hiyo haitoshi, mahakama ilipoagiza vipimo vya DNA ilibainika kuwa damu ya Douglas haiendani na ile iliyokutwa kwenye kisu kilichotumika kumchoma Olesen.

Hata hivyo, baada ya Douglas kuachiwa kwa dhamana, familia ya Olesen haijaridhishwa na hukumu hiyo. Theresa, ambaye ni wifi wa Olesen, amesema familia ina wasiwasi na hukumu iliyosomwa na mahakama.

Aidha, Theresa anasema bado hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwamba Douglas hakuwepo kwenye eneo la tukio wakati wa mauaji, hivyo alipaswa kuendelea kusota gerezani wakati kesi ikiendelea.

Licha ya kurejea uraiani kwa dhamana, Douglas amepewa masharti ya kuvaa kifaa maalumu cha ‘GPS’ ili kubaini kila anapokwenda, lengo ni kumdhibiti asitoroke wakati huu kesi ikiendelea.

Related articles

Recent articles