18.8 C
New York

Godbless Lema na kivuli cha ‘usaliti’ CHADEMA

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

KWA nyakati na nyakati, jina la Gobless Lema limekuwa likiingia na kutoka katika shutuma za usaliti ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo [CHADEMA]. Haikuanza jana na huenda hata hii ya sasa isiwe mara ya mwisho.

Kwa sasa, zipo tuhuma kwamba Lema na mtandao wake wanaendesha kampeni chafu za kusaliti mapambano ya Chama yanayoendelea wakati huu Mwenyekiti Tundu Lissu akiwa gerezani kwa mashitaka ya uhaini. Narudia, ni tetesi [taarifa zisizo na uthibitisho] tu na hazikuanza leo wala jana.

Mara zote, hasa inapotokea Lema kuibuka na mtazamo usiorandana na wa Chama, jina la ‘msaliti’ limekuwa likitangulia kuchomoza huko mitandaoni hata kabla ya hoja yake kujibiwa. Hiyo imetokea mara nyingi tu.

Mbaya zaidi, Lema amekuwa akiingia kwenye shutuma ya za aina hii ndani ya Chama kilichomlea na kumfikisha kwenye kilele cha umaarufu wa siasa za upinzani. Chama alichokitumikia kwa miaka mingi akiwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi. Kwa ufupi, Chama alichovuja jasho jingi kukipigania si tu kwake mkoani Arusha, bali nchi nzima.

Tujiulize; kwanini jina la Lema lichomoze kwenye stori za usaliti mara kwa mara? Mara nyingi anapoibuka na mtazamo unaokinzana na CHADEMA, tasfiri ya haraka huwa ni usaliti. Huenda naye hufanya hivyo akifahamu wazi matokeo yake. Turudi nyuma kidogo kuitazama historia.

Mazingira ya aina hii yaliwahi kumkuta rafiki yake kwenye siasa, Zitto Zuberi Ruyaga Kabwe. Kama alivyo Lema, Zitto naye alikuwa na ushawishi ndani ya CHADEMA lakini taswira yake ilichafuliwa mara kadhaa na shutuma za usaliti dhidi ya Chama.

Hata alipokuwa kwenye kilele cha umaarufu wake ndani ya siasa za upinzani na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA, wapo walioendelea ‘kumuua’ kwa shutuma za usaliti, kwamba alikuwa kibaraka wa Chama cha Mapinduzi [CCM] na Serikali yake. Zitto akaondoka CHADEMA.

Sasa, tofauti na ilivyo kwa Lema, mazingira ya Zitto walau yaliambatanishwa na madai ya vita ya madaraka kati yake na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama, Freeman Mbowe. Ikaelezwa kwamba alivishwa vazi la usaliti kwa makusudi baada ya wapambe wa Mbowe kujiridhisha kuwa alikuwa tishio kwenye kiti cha Mwenyekiti.

Je, mazingira hayo yapo pia kwa Lema? Ni ngumu kuyaona. Lema, licha ya ukubwa wake, humuoni akiwa amefikia levo alizokuwa nazo Zitto, linapokuja suala ya ushawishi wa ndani na nje ya Chama. Kwa ufupi, Zitto alikuwa na ‘ukubwa’ kidogo.

Kwa upande mwingine, bado utajiuliza; ni nani anayemtengenezea ‘ajali ya kisiasa’ na kwa masilahi yapi? Swali jingine; kama kweli ni msaliti, Lema anaendesha operesheni hii akiwa mstari wa mbele [kiongozi]?

Kama sivyo, kibaraka wa mtandao wa ndani au wa nje ya Chama? Nini hatima yake ndani ya CHADEMA katika siku za usoni, hasa endapo shutuma za aina hii zitaendelea dhidi yake?

Related articles

Recent articles