Na Hassan Mwasha, Gazetini
WAKATI mwingine, malalamiko ya kuchelewa kuunganishiwa huduma ya umeme kutoka TANESCO yanaweza kusababishwa na uelewa mdogo wa wateja juu ya muda stahiki wa kusubiri kuunganishwa umeme baada ya kufanya malipo.
Mathalan, wengi kati ya wateja hudhani itachukua saa chache tu baada ya kuilipia kufikiwa na mafundi na kuunganishwa umeme nyumbani au kwenye eneo lake la biashara.
Iko hivi; kwa mujibu wa Mkataba wa Huduma kwa Wateja, ikiwa mteja amelipia gharama zote na kutimiza wajibu kwa mujibu wa fomu ya maombi, muda ufuatao utazingatiwa katika kupatiwa huduma ya uunganishaji wa umeme.
Ifahamike hivi; itachukua siku 30 za kazi [achana na wikiendi au sikukuu] kwa mteja kuunganishiwa umeme ikiwa jengo lake liko umbali wa mita 30 tu kutoka iliko nguzo ya TANESCO.
Aidha, itachukua siku 60 za kazi kwa mteja ambaye jengo lake liko umbali kati ya mita 30 na mita 100. Ni kwa sababu hapo utahitaji ujezi wa njia ya nyongeza kuifikia nguzo ya TANESCO.
Hata hivyo, kama ni mfumo mpya wa usambazaji au wa umeme mkubwa kwa ajili ya biashara au kiwanda, mathalan kuweka transfoma ambalo halikuwepo, mteja atalazimika kusubiri ndani ya siku 90.
Lakini, kwa mujibu wa Mkataba wa Huduma kwa Wateja, fedha zilizolipwa na mteja na kuendelea kuwa mikononi mwa TANESCO kwa zaidi ya muda ulioelezwa hapo juu utazaa riba ya asilimia 0.5 [ya kiasi alicholipa] kila siku lakini isizidi asilimia 50 ya gharama.
Pia, Mkataba wa Huduma kwa Wateja unaweka wazi kuwa endapo TANESCO itashindwa kumuunganishia umeme mteja kwa muda uliowekwa, itawajibika kumtaarifu mapema kuhusiana na hali hiyo, na mteja atafahamishwa ni lini ataunganishiwa umeme.
Kwa maelezo zaidi, unaweza kuwasiliana na Kituo cha Huduma kwa Wateja cha TANESCO kupitia nambari 180 [bure].


