Na Hassan Mwasha, Gazetini
KWA mujibu wa Mkataba wa Huduma kwa Wateja, Shirika la Umeme nchini [TANESCO] linatoa elimu ya kutosha kwa mteja wake juu ya muda wa kusubiri kuunganishiwa umeme baada ya kufanya malipo yake.
Mteja mpya anayehitaji kuunganishiwa umeme atapaswa kufuata hatua zote muhimu za awali; kujaza fomu, kuwasilisha viambatanisho [kitambulisho cha Taifa – NIDA] na mchoro wa ‘wiring’ uliosainiwa na kutiwa muhuru na mkandarasi aliyesajiliwa.
Baada ya hapo, hatua itakayofuata ni ipi? Ni kusubiri kupokea ‘control number’ ili kulipia makadirio ya gharama za kufungiwa huduma ya umeme katika eneo lako.
Sasa, muda wa kusubiri makadirio hutegemea na umbali kati ya lilipo jengo na ilipo nguzo ya TANESCO. Kwamba si kila mteja atasubiri wiki moja au wiki mbili, bali itategemea na umbali na miundombinu ya umeme katika eneo husika.
Iko hivi; endapo umbali kati ya nguzo ya TANESCO na jengo [la kuunganishiwa umeme] ni chini ya mita 30, basi mteja aliyekamilisha hatua zote zilizotajwa hapo juu, atakuwa amepatiwa ‘control number’ na makadirio ya kiasi cha kulipia ndani ya siku 7 za kazi [pasi na kuhesabu wikiendi au sikukuu].
Kinyume cha hapo, ikiwa umbali kati ya nguzo na jengo ni mita zaidi ya mita 30 lakini hazizidi 100, basi Mkataba wa Huduma kwa Wateja unaweka wazi kuwa mteja atapatiwa makadirio ndani ya siku 10 za kazi.
Lakini, ikiwa hakuna nguzo na badala yake mfumo mpya unahitajika kujengwa katika eneo hilo, mathalan kuweka nguzo na transfoma, hasa kwa viwanda na wafanyabiashara wakubwa, makadirio ya malipo yatatolewa ndani ya siku 14 [wiki mbili] za kazi.
Je, vipi ikiwa umekidhi moja ya vigezo hivyo, mathalan uko ndani ya kundi la kwanza [ndani ya mita 30 kutoka kwenye nguzo] na hujapata control number?
Kwa maelezo zaidi, unaweza kuwasiliana na Kituo cha Huduma kwa Wateja cha TANESCO kupitia nambari 180 [bure].


