Na mwandishi wetu, Gazetini
WANANCHI wametakiwa kutambua kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hauitegemei Serikali pekee, bali unahitaji ushiriki wa kila Mtanzania kwa kutumia nafasi yake kuchangia maendeleo ya nchi.
Akizungumza na Gazetini katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mchumi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Alpha Temu, amesema Dira 2050 imeweka malengo ya kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, lakini mafanikio yake yatategemea namna wananchi watakavyotumia fursa zitakazoundwa na Serikali.
“Serikali kazi yake ni kuweka mazingira mazuri, lakini wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hizo. Kila mmoja ana wajibu wake katika kuhakikisha yale tuliyokubaliana kama taifa yanafikiwa,” amesema Temu.

Amesema tayari Julai Mosi mwaka huu Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), ambao pamoja na mambo mengine unalenga kufungua fursa za ajira, hasa kwa vijana wanaohitimu masomo na kuingia katika soko la ajira.
Kwa mujibu wake, lengo ni kufanya mageuzi ya kiuchumi yatakayoongeza uzalishaji, kukuza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje pamoja na kuhakikisha ukuaji wa uchumi unanufaisha wananchi wengi zaidi.
Tem amesema maendeleo hayo hayawezi kupimwa kwa ongezeko la pato la taifa pekee, bali pia kwa ubora wa huduma za jamii kama elimu, afya na maji.
“Hatutaki tu kujenga shule nyingi, bali tunataka kuona huduma zinakidhi viwango vya kimataifa. Vivyo hivyo kwenye maji; si kufikisha bomba tu, bali kuhakikisha wananchi wanapata maji saa 24 kila siku,” amesema.
Ameongeza kuwa Dira 2050 pia imeweka mkazo katika maendeleo yanayozingatia mazingira, matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa rasilimali ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaendelea bila kuathiri vizazi vijavyo.


