DAKAR, Senegal
MAPEMA wiki hii, Bunge la Senegal lilipitisha mabadiliko ya Katiba yaliyozua utata, yakimuondoshea madaraka makubwa aliyonayo Rais.
Hatua hiyo iliibua mgogoro mkubwa, hata polisi kulazimika kutumia mabomunya machozi kurejesha hali ya utulivu nje ya ofisi za Bunge.
Kwamba wapo wabunge waliogoma kukubaliana na mabadiliko hayo yanayotajwa kulipa nguvu kubwa Bunge dhidi ya Serikali.
Ikumbukwe, kumekuwapo na mgogoro unaotafsiririwa kuwa ni vita ya madaraka kati ya Rais Bassirou Diomaye Faye na rafiki yake wa zamani, Ousmane Sonko, ambaye sasa ni Spika wa Bunge.
Faye aliingia madarakani kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2024, kisha kumteua Sonko kuwa Waziri Mkuu wake.
Baada ya miezi mingi ya pande mbili hizo kuzozana, Sonko akikosoa namna Rais Faye unavyoshughulikia Deni la Taifa, hatimaye ‘alitumbuliwa’ Mei, 2026.
Hata hivyo, Sonko ambaye Chama chake cha Pastef ndicho chenye wabunge wengi, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge.
Katika mabadiliko ya Katiba yaliyopendekezwa na Chama hicho, Bunge litakuwa na nguvu kubwa ya kuiwajibisha Serikali, ikiwamo kutaka ikabidhiwe mkataba yote inayohusu rasilimali za nchi.
Pia, katika mapendekezo, Bunge linataka Rais aliyeko madarakani kutokuwa kiongozi wa chama cha siasa. Hiyo inamlenga Rais Faye, ambaye bado ni kiongozi wa Pastef.
Vilevile, kutaka Rais azuiwe kusaini sheria katika kipindi cha kati ya Uchaguzi na kile cha kuapishwa.
Kwa mujibu wa Pastef, Chama chenye viti 130 kati ya 165 Bungeni, kimesema mabadiliko hayo yanalenga kuleta mizania ya mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali, Bunge na Mahakama.
Lakini, wanasiasa wa upinzani waliotoka Bungeni kama ishara ya kutokuunga mkono mabadiliko, wanaona Sonko anayafanya hayo ili kulipiza kisasi cha kufukuzwa katika nafasi ya Waziri Mkuu.
Kufuatia hatua ya Bunge, Waziri wa Katiba, Moussa Sarr, alisema Rais Faye ana mpango wa kuitisha mchakato wa kura ya maoni kwa wananchi wote juu ya manadiliko.
Kauli hiyo imejibiwa na Sonko, akisema Rais hana mamlaka ya kufanya hivyo kwani mabadiliko yameshapitishwa na wabunge kama inavyopaswa kufanyika.


