29.4 C
New York

Mchezo wa kuogelea wazidi kupaa nchini, TSA  yaeleza siri ya mafanikio

Published:

Na Winfrida  Mtoi, Gazetini

MCHEZO wa kuogelea umezidi kushika kasi nchini  kutokana na kuongezeka idadi ya washiriki na wadau  kila siku, hali inayotoa picha kuwa mwamko kwa  watanzania umekuwa mkubwa  tofauti na miaka ya nyuma.

Hilo linadhibitishwa na idadi kubwa ya washiriki waliojitokeza katika mashindano ya watoto ‘ 10th Junior Championi 2026 ambayo yameanza  leo Juni 6 hadi Juni  2026  katika bwawa la kuogelea la la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Masaki jijini Dar es Salaam.

Zaidi ya waogeleaji 400 wamejitokeza  ambao ni watoto wa kuanzia miaka 6-12, waliotokea kwenye klabu mbalimbali hapa nchini, huku wageni wakitokea Zambia na Kenya.

Akizungumzia mashindano hayo, Mwenyekiti wa Chama cha mchezo wa Kuogelea Tanzania ( TSA), David Mwansyoge, amesema haijawahi kutokea kupata idadi kubwa ya washiriki kama mwaka huu.

Ameeleza kuwa siri ya mafanikio hayo ni uwepo wa misingi mizuri ya programu za junior, pamoja na ushirikiano  wa  chama  na  wadau mbalimbali, wakiwamo  wazazi na makocha.

‘Jumla ya klabu 25 zimeshiriki, ambapo klabu tano zimetoka nje ya Tanzania, zikitokea nchi za Kenya na Zambia. Sio kila mtu anaweza kushiriki,  ili ushiriki mashindano haya kuna vigezo maalum vya muda na wote waliopo hapa wamefikia,” amesema Mwenyekiti huyo.

Aidha amesema mikakati na malengo ya sasa, pia ni  kuhamasisha na kukuza uogeleaji wa kwenye bahari (Open Water) wakiwa na imani kuwa njia hiyo inaweza kuleta mafanikio kwa haraka zaidi ikilinganishwa na uogeleaji wa kwenye mabwawa (swimming pools).

Kwa upande wake kocha  Ally Msasi amebainisha kuwa kutokana na ubora  wa vijana unaonekana katika kila mashindano ni wazi Tanzania itaanza kushuhudia  medali za mashindano ya Kimataifa.

Ametolea mfano wa mafanikio yaliyopatikana hivi karibuni nchini Algeria kwenye mashindano ya Afrika ya vijana wenye umri  chini ya miaka 15-19, ambapo vijana wengi wa Kitanzania wenye umri wa miaka 13 hadi 15 walifanikiwa kutinga hatua ya fainali.

​”Wale machampioni wa Junior walioendelea  kufanya vizuri na kudumisha kiwango chao, tumeona matunda yake. Ni dhahiri kuwa, ndani ya miaka mitatu hadi minne ijayo, programu hizi zitaleta medali  nyingi nchini.” ameeleza kocha huyo ambaye anatokea  klabu ya Lake Victoria kutoka jijini Mwanza


Related articles

Recent articles