13.8 C
New York

ANC yapata ushindi kiduchu Uchaguzi Afrika Kusini

Published:

PRETORIA, Afrika Kusini

CHAMA tawala cha Afrika Kusini, African National Congress [ANC], kimepata ushindi mwembamba zaidi kuwahi kutokea tangu Nelson Mandela alipoiongoza nchi hiyo kumaliza sera ya ubaguzi wa rangi miaka mingi iliyopita.

Ni katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo ANC imepata ushindi kiduchu wa asilimia 30.76 ya kura, anguko kubwa ikilinganishwa na asilimia 46 za mwaka 2021 au asilimia 64.82 za miaka 20 iliyopita.

Kwa upande mwingine, Limpopo ndiyo jimbo pekee kati ya tisa lililoipa ANC kura nyingi katika Uchaguzi huo.

Ni tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2021, ambapo Chama hicho kilichopigania uhuru wa Afrika Kusini kilikusanya kura nyingi katika majimbo sita kati ya tisa.

Kama hiyo haitoshi, katika Uchaguzi wa safari hii, ANC imepata kura nyingi katika miji miwili pekee kati ya nane, ikilinganishwa na sita katika Uchaguzi uliopita.

Safari hii, Chama cha Democratic Alliance (DA) kimeshika nafasi ya pili kikiwa na asilimia 24.64 ya kura, huku kikiendeleza rekodi yake ya kuvuna kura nyingi katika Mji wa Cape Town.

Aidha, Chama kinachoongozwa na Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, MK, kimeshika nafasi ya tatu kikiwa na asilimia 9.76 ya kura, nyingi zikipatikana katika Mji wa Durban.

Kwa upande wake, Economic Freedom Fighters (EFF), ambacho ni Chama kinachoongozwa na mwanasiasa kijana aliyewahi kuwa kada wa ANC, kimekamata nafasi ya nne kikiwa na asilimia 6.22 ya kura.

Akizungumzia matokeo hayo, Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula, ameyaita kuwa ni janga kwa Chama hicho. “Tulijua kwamba janga linakuja. Tukiwa tunaelekea kwenye Uchaguzi, hali ya maisha ya watu wetu ilikuwa mbaya,” amesema.

Related articles

Recent articles