18.4 C
New York

Ndugu, ‘washikaji’ wanavyomfelisha Waziri Mkuu Hispania

Published:

MADRID, Hispania

WAZIRI Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez, ametimiza miaka nane tangu alipoingia madarakani, huku skendo za rushwa zikichukua nafasi kubwa katika uongozi wake kwa miaka ya hivi karibuni.

Wakati Waziri Sanchez akionekana msafi na asiye na makandokando, kashfa za rushwa zinazohusisha ndugu na marafiki zake wa karibu ndani ya Chama chake cha Kijamaa zimemchafua kwa kiasi kikubwa.

Katika hao, yumo kaka yake, ambaye pia ni mwanamuziki maarufu nchini Hispania, David, ambaye ameshafunguliwa mashitaka.

David anashitakiwa kwa kujipatia zabuni ya kazi ya kimuziki bila kupitia njia ya ushindani kutoka kwa kampuni zingine. Hata baada ya kupata, hakutekeleza majukumu yake licha ya kulipwa.

Wakati huo huo, shemeji yake, Begona Gomez, ambaye ni mke wa Waziri Mkuu, Sanchez, naye biashara zake zinachunguzwa baada ya waendesha mashitaka wa Hispania kutilia shaka mwenendo wake.

Pia, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Jose Luis Rodriguez Zapatero, ambaye naye ni mtu wa karibu wa Waziri Mkuu, naye anachunguzwa kwa tuhuma za utakatishaji fedha.

Zapatero anashutumiwa pia kwa kutumia ushawishi wake kujiingizia euro milioni 53 kutoka katika Kampuni ya ndege ya Plus Ultra mwaka 2021.

Mashitaka hayo si tu yamekichafua Chama na taswira ya Waziri Mkuu, pia yamemtia doa Zapatero, ambaye alikuwa na heshima kubwa akiwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2011.

“Kwa kuwa Waziri Mkuu mstaafu wa kwanza kuchunguzwa, ina athari mbaya (kwa Chama cha Kijamaa). Pia, ameharibu taswira yake nzuri ndani ya Chama,” amesema mchambuzi wa siasa nchini Hispania, Paco Camas.

Mwanasiasa huyo atapandishwa mahakamani Juni 17, 2026, licha ya kwamba amekuwa akisisitiza kuwa hausiki kwa lolote juu ya mashitaka yanayomkabili.

Mwaka 2023, Waziri wa Usafirishaji wa zamani, Jose Luis Abalos, alichunguzwa kwa tuhuma za kuhusika katika mauzo ya ‘mask’ zenye thamani ya Pauni milioni 43 wakati wa janga la Corona.

Haikuwa mara moja kwa Abalos. Mwaka 2025, mwanasiasa huyo mwandamizi alitajwa kuomba na kupokea rushwa ili kusaini baadhi ya mikataba, akishirikiana na rafiki yake ndani ya Chama, Santos Cerdan.

Kwa wakati wote huo wa kashfa, Waziri Mkuu alikuwa upande wa vigogo hao wa Chama, hadi alibadili mawazo baada ya Mahakama kuwakuta na hatia.

Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni taswira ya Waziri Mkuu ilitikiswa tena na tukio la polisi kuzivamia ofisi za Makao Makuu ya Chama kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Ni baada ya taarifa kuwa Chama kilimlipa kiasi cha fedha mwanachama wake, Leire Diez, ili kuendesha kampeni kubwa ya kuwachafua polisi, mahakimu na waendesha mashitaka wanaochunguza kesi zilizopo.

Ni kutokana na mfululizo wa kashfa hizo, sasa wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakishinikiza hatua ya Waziri Mkuu, Sanchez, kujiuzulu na kuitisha Uchaguzi, kabla ya Serikali yake kuanguka.

Hata hivyo, Waziri wa Usafirishaji wa sasa, Oscar Puente, ameziita kesi zilizopo kuwa ni njia za wapinzani kutaka kuingia Ikulu bila kutumia boksi la kura.

“Kuna watu wanataka kuangusha Serikali, kisha waingie madarakani kwa njia zisizo halali, zisizo za kidemokrasia,” amesema.

Kwa upande wake, kiongozi wa Chama cha upinzani cha People’s Party (PP), Alberto Nunez Feijoo, amesema kashfa zilizopo ni kielelezo cha kuishiwa nguvu kwa Serikali iliyoko madarakani.

Aidha, madai hayo yamemfikia Waziri Mkuu, Sanchez, ambaye naye amejibu akisema hayuko tayari kujiuzulu, na badala yake atamaliza awamu yake inayokomea mwaka 2027.

Related articles

Recent articles