Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Mwanza
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI imezindua rasmi programu ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa elimu katika shule za sekondari nchini.
Programu hiyo inayotekelezwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Tanzania (ADEM) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (VVOB), itatekelezwa katika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza Mei 28, 2029 katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Mwanza, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dk. Maulid Maulid, amesema zaidi ya viongozi wa elimu 16,000 watanufaika na programu hiyo, wakiwemo wakuu wa shule za sekondari 12,000 pamoja na wasaidizi wao na waratibu elimu zaidi ya 4,000 nchini kote.
Dk. Maulid amesema programu hiyo imelenga kuwajengea uwezo viongozi hao katika maeneo ya uongozi wa kimkakati, misingi ya utawala bora shuleni, maadili ya ualimu, usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na matumizi ya TEHAMA katika uongozi wa elimu.
“Mwaka 2015 ndiyo ilikuwa mara ya mwisho ADEM kuendesha mafunzo makubwa ya uongozi kwa wakuu wa shule za sekondari kitaifa. Tangu wakati huo viongozi wengi waliopata mafunzo wamestaafu au wamepanda vyeo, hivyo kizazi kipya hakikupata mafunzo rasmi ya uongozi,” amesema Dk. Maulid.

Kwa upande wake, Meneja wa Programu kutoka VVOB, Sarish Haribae, amesema programu hiyo itatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030 ili kuendana na mabadiliko ya sekta ya elimu duniani.
Akizindua programu hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema mpango huo utaimarisha mfumo wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA).
“Sekta ya elimu haiwezi kupata mabadiliko ya kweli kama watendaji wake hawatawezeshwa kuendana na maboresho ya sera mpya ya elimu,” amesema Prof. Nombo.


