21.9 C
New York

Hesabu tu! Mechi 5 zilizoamua ubingwa wa Arsenal

Published:

LONDON, Uingereza

BADO mashabiki wa Arsenal hawajamaliza furaha yao. Ukame wa miaka 22 wa kulikosa taji la Ligi Kuu ya England (EPL) umefikia ukomo msimu huu wa 2025-26 na sasa ni mabingwa wapya wakiwa na mechi moja mkononi.

Kwa upande mwingine, makala haya yanakuchambulia mechi 5, ambazo matokeo yake yaliiweka Arsenal katika nafasi nzuri ya kuwa mabingwa. Endelea kusoma …

MAN UNITED 0-1 ARSENAL (AGOSTI 17, 2025)

Ni mechi ya wikiendi ya kwanza ya msimu na Arsenal walikwenda Old Trafford wakiwa na kumbukumbu mbaya ya ‘kupoteana’ mara nyingi walizocheza katika Uwanja huo.

Safari hii, walionesha kuwa wako tofauti. Arsenal walipata bao pekee ndani ya dakika ya 13 tu ya mchezo huo kupitia kwa beki wao wa pembeni, Riccardo Calafiori, aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na kiungo Declan Rice.

Kiwango bora cha safu ya ulinzi chini ya William Saliba, Gabriel Magalhaes na kipa wao, David Raya, kilitosha kutuma ujumbe kuwa Arsenal ya msimu huu ilikuwa imejipanga kunyakua ubingwa.

NEWCASTLE 1-2 ARSENAL (SEPT. 28, 2025)

Washika Bunduki waliingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi tatu mfululizo walizokwenda ugenini kuifuata Newcastle United.

Katika dakika ya 34, Newcastle walitangulia kwa bao la Nick Woltemade lakini Arsenal waliendelea kutawala mchezo na hatimaye Mikel Merino aliisawazishia Arsenal katika dakika ya 84.

Wakati mashabiki wa Newscastle wakiamini mechi imekwisha kwa sare, Gabriel aliifungia Arsenal bao la ‘dakika za jioni’ na kuwapa pointi tatu za ugenini.

ARSENAL 2-0 EVERTON (MACHI 14, 2026)

Kuelekea mechi hiyo, kocha Mikel Arteta alikuwa na msongo wa mawazo kutokana na wimbi la majeruhi katika kikosi chake, huku Man City ikiendelea kumpa presha kwenye msimamo wa Ligi.

Ndani ya uwanja, Everton walikuwa wa moto. Kipa wao, Jordan Pickford, alikuwa kwenye ubora wake wa kuokoa mabao, wakati huo pia Dwight McNeil akiikosa Arsenal mara kadhaa.

Mambo yalibadilika baada ya Arteta kufanya mabadiliko kipindi cha pili. Viktor Gyokeres na kinda Max Dowman, ambao kila mmoja alifunga bao moja kubakiza pointi tatu pale Emirates.

MAN CITY 2-1 ARSENAL (APRILI 19, 2026)

Kupoteza mechi hii kwa mabao ya Rayan Cherki na Erling Haaand kilikuwa ni kipimo cha ukomavu wa Arsenal. Wengi waliamini matokeo hayo yangeipoteza moja kwa moja, na badala yake yaliwaimarisha kisaikolojia.

Ni kuanzia hapo, Arteta na vijana wake waliona hakuna namna ya kuupata ubingwa bila kushinda mechi zilizobaki mbele yao. Kichapo hicho kiliongeza morali kikosini.

Kwa tafsiri rahisi, huenda kuifunga Man City kungewafanya wachezaji wa Arsenal ‘wa-relax’, kama ambayo wamekuwa wakifanya katika mechi za mwisho kwa misimu mingi ya hivi karibuni.

WEST HAM 0-1 ARSENAL (MEI 10, 2026)

Kutokana na hali mbaya waliyonayo West Ham United kwenye msimamo wa Ligi, ilitarajiwa kuwa mechi ngumu kwa Arsenal, ikizingatiwa kuwa walikuwa ugenini Magharibi mwa Jiji la London.

Licha ya kuiruhusu kumiliki mpira kwa sehemu kubwa, West Ham United iliizua kwa sehemu kubwa mipango ya Arsenal kutengeneza nafasi za kufunga.

Ni hadi ilipofika dakika ya 83, ndipo Washika Bunduki waliposhangilia bao kupitia kwa nyota wao raia wa Ubelgiji, Leandro Trossard. Arsenal wangeweza kukosa pointi tatu, kama si VAR kulikataa bao la kusawazisha la Callum Wilson.

Related articles

Recent articles