18.5 C
New York

Pete Hegseth: Mtaalamu wa vita anayempa jeuri Donald Trump

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KWA sasa ndiye ‘Katibu wa Vita’, jina ambalo amepewa na Rais Donald Trump. Kiuhalisia, Pete Hegseth ni Katibu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani.

Wanaomfahamu Hegseth watakumbuka kuwa aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Fox News.

Akiwa hapo, alifanya kazi nzuri na iliyomvutia Trump na wafuasi wake wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita uliomrudisha madarakani.

Hegseth anafahamika kwa matamko yake mazito. Wiki chache zilizopita, alisema Marekani haitakuwa na huruma kwa adui yake yeyote katika vita inayoendelea dhidi ya Iran.

Kwa upande, Hegseth amekuwa akikosolewa na wakati mwingine wapinzani wake kumuhusisha na uhalifu wa kivita.

Wakosoaji wake wanatolea mfano kilichofanywa na vikosi vya kijeshi vya Marekani nchini Venezuela, wakisema Hegseth ndiye aliyeamrisha yafanyike ‘maangamizi ya kutisha’.

Baadhi ya maangamizi hao ni kushambuliwa kwa boti za Venezuela, ambapo raia kadhaa wa nchi hiyo waliuawa kwa madai ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mara zote Hegseth amekuwa akiweka wazi kuwa atapigania masilahi ya Marekani kwa namna na njia yoyote ile.

Mwaka 2024, wakati huo akiwa hajawa Katibu wa Ulinzi, aliwakingia kifua wanajeshi wa Marekani waliokuwa wakikabiliwa na mashitaka ya uhalifu wa kivita.

Alizaliwa mwaka 1980 huko Minneapolis-Saint Paul, Minnesota. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alisomea siasa katika Chuo Kikuu cha Princeton.

Alipohitimu chuo kikuu, Hegseth alijiunga na jeshi mwaka 2023 na kufanya kazi katika Gereza la Guantanamo nchini Cuba, kabla ya kupelekwa Iraq na Afghanistan.

Baadaye, alipanda cheo na kuwa Meja, wakati huo pia akiwa mchambuzi na mtangazaji wa Fox News, kazi iliyompa umaarufu mkubwa nchini Marekani.

Licha ya uteuzi wake wa nafasi ya Katibu wa Wizara ya Ulinzi kupingwa na baadhi ya wanasiasa wa Chama cha Trump, Republican, bado kiongozi huyo wa nchi alisisitiza kuwa Hegseth ndiye mtu sahihi.

Trump alimzungumzia Hegseth akisema: “Pete ni shupavu, ana akili na ni muumini mkubwa wa masilahi ya Marekani (America First).”

Katika ulingo wa siasa, Hegseth hana ukomavu wa kutosha. Mwaka 2012, alijaribu kugombea nafasi ya Seneta kupitia Chama cha Republican lakini alijitoa kwenye kinyang’anyiro.

Alikuwa Rais wa Chama cha Maveterani wa jeshi lakini wengi wao walipinga kitendo cha Trump kumteua kuwa Katibu wa Masuala ya Maveterani mwaka 2016.

Kwa upande mwingine, wapo wanaosema Hegseth si muumini wa usawa wa kijinsia. Kwamba aliwahi kusema wanawake hawapaswi kupewa baadhi ya nafasi jeshini.

Katika hatua nyingine, aliwahi kuibuka mwanamke aliyedai kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia na Hegseth mwaka 2017.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img