13.9 C
New York

Jeffrey Epstein; Mwalimu wa Hisabati aliyewaingiza matatani akina Trump

Published:

LOS ANGELES, Marekani

WA sasa, siasa za dunia zinatikiswa na kile kinachoitwa ‘mafaili ya Epstein’. Ni taarifa za siri zilizoibuka baada ya Jeffrey Epstein kufariki miaka saba iliyopita.

Epstein alipoteza maisha Agosti 10, 2019, wakati huo akiwa katika Gereza la New York, Marekani, akisubiri kuhukumiwa baada ya mashitaka ya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake.

Alikuwa akihusishwa na mtandao haramu wa kusafirisha wanawake na wasichana kwa ajili ya biashara ya ngono.

Kwamba alikuwa akivuna fedha nyingi kwa kuwaunganisha wanawake hao na wafanyabiashara, wanasiasa na watu wengine maarufu.

Ikiwa ni miaka saba tangu Epstein alipofariki, zimeibuka taarifa nyingi (mafaili ya Epstein) zinazohusisha ukaribu wake na watu maarufu, wakitajwa kuwa huenda nao walikuwa wakinufaika na huduma yake ya biashara aliyokuwa akifanya.

Epstein ni nani?

Alizaliwa mjini New York na aliwahi kuwa mwalimu wa masomo ya Hisabati na Fizikia wa Shule binafsi ya Sekondari ya Dalton. Hiyo ni katika miaka ya 1970.

Baadaye, mmoja ya wazazi wa wanafunzi wake alimpa ‘koneksheni’ ya biashara ya hisa katika Benki ya Bear Stearms.

Kupitia kampuni yake ya J Epstein and Co, alianza kupata mafanikio makubwa, yakionekana wazi baada ya kununua nyumba za kifahari katika miji ya Florida, New York na hata nje ya Marekani.

Ni kuanzia hapo, Epstein alianza kuwa karibu na watu maarufu, wakiwamo wasanii na wanasiasa wa Marekani.

Mikasa yake

Epstein alijijengea taswira ya mtu anayependa maisha ya ‘kujirusha’. Aliandaa hafla nyingi nyumbani kwake na katika migahawa na hoteli mbalimbali, huku akiwaalika watu wenye majina makubwa.

Lakini, mwaka 2005, wazazi wa binti mwenye umri wa miaka 14 walimfungulia mashitaka Epstein wakidai kuwa amemdhalilisha kingono binti yao.

Kwa mujibu wao, Epstein alifanya hivyo akiwa na binti huyo katika nyumba yake ya kifahari iliyoko katika fukwe za Palm.

Polisi walipofika katika mjengo huo kwa ajili ya upekuzi, walibaini kuwapo kwa picha nyingi za wasichana wenye umri mdogo.

Mwandishi wa habari maarufu, Michael Wolff, alifichua mazungumzo yake na Epstein akisema mfanyabiashara huyo aliwahi kumwambia kuwa anapenda wasichana.

“Wakati fulani, wakati kashfa zake zinaanza kufichuka, nilikuwa nazungumza naye na aliniambia ‘sina cha kusema, napenda wasichana wadogo’,” anasema Wolff katika mahojiano yake na Jarida la New York mwaka 2007.

Waliotajwa kashfa zake

Rais wa Marekani, Donald Trump, ni miongoni mwao. Trump amewahi kukiri kuwa na ukaribu na Epstein, ingawa anakana kuhusika katika uhalifu wake.

Taarifa zinadai kuwa Trump aliwahi kumfukuza Epstein katika klabu yake baada ya mfanyabiashara huyo kumdhalilisha mmoja ya wahudumu wa kike.

Mwaka 2002, Epstein alitumia ndege yake kumsafirisha Bill Clinton (Rais wa zamani wa Marekani) hadi barani Afrika. Ni safari iliyowahusisha pia waigizaji Kevin Spacey na Chris Tucker.

Mwingine kwenye listi ya ‘marafiki’ wa Epstein, ingawa haimaanishi moja kwa moja kuwa nao ni wahusika, ni bilionea wa Marekani, Elon Musk.

Katika mafaili ya Epstein, imenaswa barua-pepe (email) yenye mazungumzo yao wakipanga juu ya Musk kuhudhuria sherehe aliyoandaa Epstein.

Bill Gates, bilionea mwingine wa Marekani, naye ameibuliwa na mafaili ya Epstein. Barua-pepe mbili za mazungumzo yao zimenaswa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Slovakia, Miroslav Lajcak, naye yumo. Ni baada ya mazungumzo yake na Epstein yaliyofanyika kwa barua-pepe kunaswa.

Katika mazungumzo yao, Lajcak anamlaumu Epstein kwa kutokumualika katika sherehe zake. Katikati ya mazungumzo, Lajcak anaulizia uwezekano wa kupewa binti wa ‘kupumzika’ naye, jambo ambalo anahakikishiwa na Epstein.

Ni kutokana na kashfa hiyo, Lajcak amejiuzulu nafasi aliyokuwa nayo hivi karibuni ya Mshauri wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Slovakia.

Ehud Barak, ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak, naye jina lake limechomoza katika kashfa hii ya Epstein.

Barua-pepe za mazungumzo yao ya mwaka 2008 zimeibuliwa. Licha ya kukiri ukaribu wake na Epstein, Barak amesema si tu hajui chochote kuhusu ‘uhuni’ wa Epstein, bali pia hajawahi kuhudhuria sherehe zake.

Anusurika kifungo cha maisha

Hata hivyo, licha ya kukutwa na hatia katika mashitaka mengi ya aina hiyo, Epstein alihukumiwa kifungo cha miezi 18 pekee.

Wakati huo, ilielezwa kuwa alitoa rushwa kupunguziwa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani.

Cha kushangaza, huku akitumikia kifungo, bado Epstein aliruhusiwa kuendelea na kazi zake, ambapo alipewa saa 12 kwa siku kwenda ofisini kwake.

Aliachiwa baada ya miezi 13, kabla ya kukamatwa tena safari hii, ambapo hata hivyo alifariki akiwa anasubiri hukumu mwaka 2019.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img