KAMPALA, Uganda
YOWERI Museveni anayewania muhula wake wa saba madaakani anaongoza katika majibu ya awali ya Uchaguzi Mkuu wa Uganda uliofanyika jana.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume leo Ijumaa Januari 16, 2026, Museveni yuko mbele kwa asilimia 76 ya kura.
Matokeo hayo ni asilimia 45 ya vituo, ambapo mpinzani wake wa karibu katika kinyang’anyiro cha urais, Bobi Wine, amepata asilimia 20 tu ya kura.
Museveni ana umri wa miaka 81 na amekuwa Rais wa Taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka 1986. Wengi wanakosoa kitendo chake cha kung’angania Ikulu.
Pia, wakosoaji wake wamekerwa na kitendo cha Serikali ya Uganda kuzuia upatikanaji wa mitandao (intaneti), wakisema ni sehemu ya njama za wizi wa kura.
Kwa upande wake, Bobi Wine (43), ameweka wazi kuwa atahamasisha maandamano ya nchi nzima kupinga matokeo endapo atajiridhisha kuwa Museveni ameiba kura za kumbakiza madarakani.


