RABAT, Morocco
MATAIFA mawili makubwa katika soka yatavaana Jumamosi hii ya Januari 10, 2026, ukiwa ni mchezo wa robo fainali ya msimu huu wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).
Ni timu zinazokutana, huku kila moja ikiwa imeshinda mechi zake zote nne za mashindano hayo. Pia, kila moja ilivuka hatua ya makundi ikiwa kileleni mwa kundi.
Mechi itachezwa katika Uwanja wa Marrakech, ambapo timu itakayopata ushindi itatinga nusu fainali.
Kwa upande mwingine, timu hizo zinakutana zikiwa na sura tofauti katika maeneo ya ulinzi na ushambuliaji.
Nigeria ‘Super Eagles’ ni hatari kwenye eneo la mwisho (ushambuliaji) ikiwa imefunga mabao 12, wakati Algeria ni bora katika safu ya ulinzi iliyoruhusu bao moja pekee.
Licha ya uimara wa ‘ukuta’ wao, mabeki wa Algeria watakuwa na kibarua kizito cha kuikabili safu ya ushambuliaji ya Eagles inayoongozwa na Victor Osimhen.
Straika huyo wa Galatasaray ameshafunga mabao matatu na kutoa ‘asisti’ moja katika mechi nne pekee za msimu huu wa AFCON.
Pia, safu ya ushambuliaji ya Eagles inaye staa wa Atalanta ya Serie A, Ademola Lookman, ambaye amepasia nyavu mara tatu na kutoa asisti nne.
Lakini, mabeki wa Eagles nao watapaswa kumchunga kwa dakika zote za mchezo nahodha wa Algeria, Riyad Mahrez. Ana mabao matatu.
ia, washambuliaji wa Eagles watakuwa na kibarua kigumu kuziona nyavu za Algeria zinazolindwa na kipa wa Granada ya Hispania, Luca Zidane.
Kwa makipa wote wa kikosi cha kwanza walioko robo fainali, mtoto huyo wa Zinedine Zidane ‘Zizou’ ndiye pekee ambaye haijaruhusu bao msimu huu wa AFCON.
Kuelekea mchezo huo, Algeria wana rekodi ya kushinda mara nne, kufungwa tatu na kutoa sare mbili katika mechi tisa walizokutana na Eagles.
Kumbukumhu mbaya zaidi waliyonayo Eagles katika mechi walizokutana na Algeria ni kichapo cha mabao 5-1 mwaka 1990.


