RABAT, Morocco
TIMU ya soka ya taifa ya Senegal imetinga robo fainali ya msimu huu wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) kwa kuifunga Sudan mabao 3-1 katika mchezo wa hatua ya 16 Bora uliochezwa jana Januari 3, 2025.
Hata hivyo, stori kubwa ni Ibrahima Mbaye aliyetokea benchi na kufunga bao la tatu (dk. 77) baada ya Pape Gueye kuzifumania mara mbili nyavu za Sudan.
Kwa bao hilo, Mbaye wa PSG anakuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga katika mechi za AFCON tangu Mikel Obi wa Nigeria alipofanya hivyo miaka 20 iliyopita.
Obi aliweka rekodi hiyo akiwa na miaka 18, miezi tisa na siku tano, alipoitungua Zimbabwe katika mechi yake ya kwanza akiwa na ‘uzi’ wa Super Eagles.
Kama alivyofanya Mbaye, Obi aliyewahi kupita Chelsea naye alifunga bao akitokea benchi kuchukua nafasi ya Wilson Oruma.
Akitumia dakika chache uwanjani, aliachia shuti lililomshinda kipa wa Zimbabwe na kuiwezesha Eagles kupata ushindi wa mabao 2-0.


