RABAT, Morocco
ACHANA na kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Nigeria jana Desemba 31, 2025. Pia, sahau kuhusu kuishia hatua ya makundi ya fainali za msimu huu za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).
Timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ inaweza kuwa ya kwanza katika historia ya michuano hiyo kutumia makipa wote watatu, tena ndani ya dakika 11 tu.
Dhidi ya ‘Super Eagles’, Uganda ilianza na kipa mkongwe, Dennis Onyango, lakini alitolewa mapema kabisa baada ya kuumia enka akijaribu kumzuia Paul Onuachu.
Kipa namba mbili, Salim Magoola, aliingia mwanzo mwa kipindi cha pili lakini tukio lake la kutoka nje ya boksi na kumchezea rafu Victor Osimhen lilimsababishia kadi nyekundu.
Hiyo ilisababisha benchi la ufundi la The Cranes kumtoa kiungo Baba Al Hassan ili kumpa nafasi kipa chaguo la tatu, Nafian Alionzi.
Dakika tatu tu baada ya Alionzi kuingia, ndipo Eagles walipofunga bao la pili kupitia kwa Raphael Onyedika, ambaye pia ndiye aliyefunga tena dakika tano tu baadaye.


