22 C
New York

Matukio muhimu siasa za Afrika 2025

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

HAKIKA ulikuwa ni mwaka wa kashikashi nyingi katika uga wa siasa barani Afrika. Ndiyo, ni mwaka 2025.
Ni yapi matukio yaliyoacha alama kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita? GAZETINI inachambua kwa msaada wa mashirika ya habari ya kimataifa.

Uchaguzi Mkuu Tanzania

Kwa mara ya kwanza katika historia ya siasa za Tanzania, Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 uligubikwa na machafuko yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali kwa baadhi ya maeneo.

Pia, ni kwa mara ya kwanza, mgombea wa kiti cha urais kupata ushindi mnono wa asilimia 98 ya kura. Ni Samia Suluhu Hassan wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika nchi jirani ya Malawi, Rais wa zamani, Peter Mutharika, aliteka vichwa vya habari barani Afrika baada ya kurejea madarani.

Visiwa vya Ushelisheli nako kulikuwa gumzo mwaka 2025 baada ya Chama tawala cha zamani, United Seychelles, kurudi madarakani baada ya miaka mitano ya upinzani kuongoza nchi.

Kwa upande wa Afrika Kusini, Chama tawala cha African National Congress (ANC) kilishuhudiwa kikipata kura chache zaidi katika historia ya siasa za nchi hiyo na kusababisha iunde Serikali ya Umoja kwa kushirikiana na upinzani.

Wakati huo huo, maandamano makubwa yalichomoza nchini Senegal baada ya jaribio la rais kutaka kuongeza muda wa kubaki madarakani.

Uchaguzi ulifanyika na hatimaye mgombea asiye na jina kubwa katika siasa za Taifa hilo alishinda, ingawa yule mwenye ushawishi mkubwa wa upinzani alizuiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu.

Aidha, ni katika kipindi hicho cha mwaka 2025, mataifa ya Mali, Niger na Burkina Faso yalitangaza kujitoa katika Jumuhiya ya Uchumi kwa nchi za Afrika ya Magharibi (ECOWAS).

Na badala yake, majirani hao waliunda Umoja wao unaoundwa na serikali zilizoko madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi.

Nchini Cameroon, licha ya vijana kuwa ndiyo idadi kubwa ya raia, Paul Biya mwenye umri wa miaka 92, aliwashangaza wengi alipotangaza kugombea kiti cha urais.

Hatimaye, Biya ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 43, alishinda na kuingia Ikulu kwa muhula wake wa tisa.

Septemba, liliibuka vuguvugu la maandamano makubwa ya vijana katika Kisiwa cha Madagascar wakishinikiza Serikali iliyoko madarakani kujiuzulu.

Ili kujinasua, Andry Rajoelina alijaribu kuvunja baraza la mawaziri lakini haikusaidia. Bado vijana waliandamana wakitaka naye kuachia madaraka.

Ni kutokana na vuguvugu hilo, Rajoelina aliondolewa kwa mapinduzi ya kijeshi yaliyomtangaza Michael Randrianirina kuwa rais wa mpito.

Mazingira ya aina hiyo yalikaribia kutokea nchini Benin, kabla ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi kugonga mwamba.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img