BAMAKO, Mali
KAMA ambavyo Marekani iliweka marufuku kwa raia wa Mali na Burkina Faso kuingia nchini humo, mataifa hayo nayo yamejibu mapigo.
Mali na Burkina Faso zimetangaza rasmi kuwa zitaweka marufuku kwa raia wa Marekani kuingia katika nchi hizo.
Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Nje ya Burkina Faso, Karamoko Jean-Marie Traore, amesema wanaangalia uwezekano wa kufanya kile kilichofanywa na utawala wa Rais Donald Trump.
Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali imesema kuzuia raia wa Marekani kuingia nchini mwao ni katika kutafuta heshima na usawa.
Aidha, Serikali ya Mali imesema ilishangazwa na hatua ya Marekani kwani haikutanguliwa na mazungumzo wala taarifa.
Hatua ya Mali na Burkina Faso kutangaza nia hiyo inakuja baada ya taarifa zinazodai kuwa Niger imeshaweka marufuku ya raia wa Marekani kuingia nchini humo.
Niger, kama zilivyo Mali na Burkina Faso, ni matafa yanayoongozwa na viongozi wa kijeshi baada ya mapinduzi ya kuondosha serikali za kiraia.


